Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya vifo na uharibifu, watoto wa kipalestina kurejea shule

Mtoto huyu wa kipalestina asimama nje ya nyumba iliokuwa nyumba yao iliyoharibiwa baada ya mashambulizi ya angani kambini mji wa Rafhakusini mwa Ukanda wa Gaza (Julai 12)© UNICEF/NYHQ2014-0911/El Baba

Licha ya vifo na uharibifu, watoto wa kipalestina kurejea shule

Zaidi ya watoto 500,000 wa kipalestina wanarejea shule wiki ijayo licha ya kwamba wengi wao hawatakuwa na maeneo ya kusomea kwa kuwa shule bado zinatumiwa na familia kama maeneo ya hifadhi kutokana na mashambulizi Israel huko Ukanda wa Gaza. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema takwimu za wizara ya elimu ya Palestina zinaonyesha kuwa shule 25 za serikali ziliharibiwa kabisa na angalau nyingine 207 ikiwemo 75 zinazoendeshwa na shirika la kuhudumia wapalestina, UNRWA zilipata uharibifu kidogo.

UNICEF inasema itakarabati shule 108 katika miezi sita ijayo kutegemea upatikanaji wa fedha.

Hata hivyo imesema pamoja na mazingira duni ya shule, watoto wanarejea shuleni wakiwa na matatizo ya kisaikolojia kutokana na vifo, ghasia na uharibifu walioshuhudia wakati wa siu 50 za mapigano.

Lakini hali Gaza ikoje hivi sasa, Jens Laerke ni msemaji wa ofisi ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA.

“Bado kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani 63,000 wanaoishi kwenye shule 29 za UNRWA huko Gaza. Wakimbizi wengine 50,000 wanaishi na wenyeji.wadau wa usaidizi wanasema fedha zaidi zahitajika kuimarisha mpango wa kusaidia wenyeji wanaohifadhi familia. Jana iliripotiwa kuwa asilimia 90 ya miundombinu ya afya imerejea ijapokuwa kuna huduma hazipo kutokana na uharibifu.Hata hivyo bado kuna changamoto kutokana na uhaba wa umeme, dawa muhimu na vifaa tiba.”

Takribani wapalestina 2,132 miongoni mwao watoto 501 waliuawa wakati wa mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Israel dhidi ya Palestina kwenye ukanda wa Gaza kwa siku 50 hadi sitisho la mapigano lilipopatikana tarehe 26 mwezi uliopita.