Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya kutisha yanafanyika kila siku Syria:Ripoti

Wakimbizi wa Syria Picha@UNHCR

Mauaji ya kutisha yanafanyika kila siku Syria:Ripoti

Kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kumaliza mzozo wa Syria kumesababisha kuzuka kwa makundi yenye mirengo mikali nchini Iraq ambayo vitendo vyake vinatishia usalama wa eneo zima la Mashariki ya Kati.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Kamishna wa tume ya kikimataifa ya uchunguzi kwa ajili ya Syria.

Ripoti hiyo imesema kundi la ISIL linalotaka kuunda dola ya Kislamu nchini Iraq ISIL limefanya uharibifu mkubwa dhidi ya binadamu katika maeneo ya Aleppo na kwinginenko kwa kuendesha vitendo kama mauaji, utesaji na kuwaandikisha watoto kwenye vikosi vya kijeshi.

Halikadhalika imeishutumu serikali ya Syria kwa kuendesha vitendo vya uhalifu wa kivita na dhidi ya kibinadamu huku watendaji wakikwepa sheria.

Mathalani imesema kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu, mamia ya wanawake na wanaume pamoja na watoto wamekuwa wakiuawa kila wiki kutokana na makombora yanayorushwa hovyo na vikosi vya serikali kwenye maeneo ya raia.

Paulo Pinheiro ni Mwenyekiti wa Tume hiyo.

(Sauti ya Paulo)

"Ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa imeshindwa kabisa katika moja ya majukumu nyeti manne ya kulinda raia. Kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu ni wazi kuwa kundi la waislamu wenye msimamo mkali wanaotaka kuunda dola ya kiisalamu, ISIS linakuwa. Linatafuta kuangamiza ubinadamu, kuangamiza raia, makundi madogo, na haki za kimsingi za wanawake na watoto. Miongoni mwa matokeo mabaya katika ripoti hii ni kambi kubwa za mafunzo ambamo watoto hususan wavulana wa miaka 14 wanahusishwa kupigana katika kundi la ISIS pamoja na watoto. Tunakaribisha hatua za ugawaji misaada Syria lakini misaada ya  kibinadamu haiwezi kufidia mateso ya kifo, uwekwaji vizuizini na majeruhi yanaoendelea."

Tume imetaka usafirishaji wa silaha kwa pande zinazokinzana Syria unapaswa kusitishwa mara moja kwani silaha hizo zinatumika kutekeleza uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu.