Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatolea wito ufadhili zaidi wakati tatizo la wakimbizi wa Sudan Kusini likiongezeka

Kundi la wakimbizi wa ndani wakiwemo wanawake na watoto wakipumzika katika eneo la Ethiopia baada ya kuvuka mto wa Baro kutoka Sudan ya Kusini. Picha: UNHCR/L.F.Godinho(UN News Center)

UNHCR yatolea wito ufadhili zaidi wakati tatizo la wakimbizi wa Sudan Kusini likiongezeka

Shirika la kuhudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR na wadau wanaokabiliana na tatizo la wakimbizi kufuatia kuzorota usalama Sudan Kusini wametoa ombi jipya la dola milioni 658 ili kusaidia wakimbizi takriban 715,000 mwishoni mwa mwaka huu wa 2014. Taarifa kamili na John Ronoh.(Taarifa ya Ronoh)

Mzozo huo unaoshuhudiwa na hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo changa kabisa duniani, umesababisha wakimbizi kukimbilia nchi jirani za Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda katika viwango vya juu kuliko ilivyotarajiwa awali. Idadi hii ya wakimbizi zaidi ya laki saba ni zaidi ya ongezeko maradufu lililotarajiwa wakati ombi la ufadhili lilipotolewa mwezi Machi.

Ethiopia imepokea wakimbizi wengi zaidi katika kipindi cha miezi michache iliyopita huku wakimbizi wapatao 11,000 wakivuka mpaka katika mji wa Burubiey katika kipindi cha masaa 72, kileleni mwa watu kukimbia mwezi Mei. Licha ya kwamba idadi hii imepungua, bado mpakani mwa Ethiopia wanapokea wakimbizi 1,000 kwa siku, mzigo ambao unadhoofisha utoaji huduma. Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR Geneva.

“Tunatoa wito wa ombi la fedha kwa dharura ili kuwasaidia watu walioko nchi jirani, na kusaidia watoto wanaofika pekee yao na watoto 14,00 waliotengana na familia zao. Kufikikia leo tumepokea ufadhili lakini ni asilimia 24 tu ya ombi ”