Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na Marekani zatoa wito kwa usaidizi wa Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya na Marekani wametoa wito wa pamoja wa kusaidia wananchi wa Sudan Kusini ambao mapigano yaliyoanza nchini mwao tarehe 15 Disemba mwaka jana yanazidi kuwaletea machungu na kusababisha zaidi ya wananchi Milioni Moja wamekimbia makazi yao na maelfu wakisaka hifadhi Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudan.
Ombi hilo la pande tatu la usaidizi limezinduliwa huko Washington DC ambapo Msimamizi Mkuu wa masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Valerie Amos amesema mapigano hayo yamesababisha uharibifu wa miji, uchumu kutwama, halikadhalika uzalishaji wa chakula.
Kwa mantiki hiyo pande tatu hizo zimetaka hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo kusitisha mapigano, pande zote kwenye mzozo wa Sudan Kusini kuheshimu sheria za kimataifa za usaidizi wa binadamu na fedha za usaidizi zipatikane ndani ya miezi mitatu ili kukidhi mahitaji ya wananchi waliosaka hifadhi ndani na nje ya nchi yao.