Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaanza uchunguzi wa awali huko Jamhuri ya Afrika ya Kati: ICC

Tunaanza uchunguzi wa awali huko Jamhuri ya Afrika ya Kati: ICC

Mwendesha mashtaka mkuu kwenye Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai huko The Hague Uholanzi, Fatou Bensouda ametangaza kufungua upya kwa uchunguzi wa kile kuendelea huko Jamhuri ya Afrika kati, CAR kutokana na tuhuma zinazoibuka kila uchao juu ya madhila ya mateso yanayokumba raia.

Katika taarifa yake hii leo Bi. Bensouda ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na mauaji ya mamia ya watu, ubakaji na utumwa wa kingono, uharibifu wa mali, mateso, watu kulazimishwa kuhama makazi yao na hata utumikishaji wa watoto kwenye vikundi vyenye silaha. Amesema katika matukio mengi, raia wanalengwa kwa kuzingatia imani zao za kidini.

Bi. Bensouda amesema tuhuma hizo na mazingira yaliyoonekana yamedhihirisha kukidhi vigezo vya ofisi yake kuingilia kati na kuchunguza na kwamba ni tofauti na wakati ule serikali ya CAR ilipowasilisha suala la uchunguzi mbele ya ICC Disemba mwaka 2004.

(Sauti ya Bensouda)

Hivyo basi nimeamua kufungua uchunguzi wa awali wa suala hili. Kwa mantiki hiyo basi jitihada za baadaye za ofisi yangu zitalenga kukusanya na kuchunguza taarifa zote muhimu kubaini iwapo kuna misingi stahili ya kuendeleza uchunguzi dhidi ya suala hili jipya.

Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC amesema jitihada zake nchini CAR kufuatilia suala hilo zitaratibiwa na Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika.

CAR ni mwanachama wa mkataba wa Roma ulioanzisha ICC.