Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule nyingi CAR bado zimefungwa:UNICEF

Mwitikio wa shule ulikuwa mkubwa pindi muhula wa shule ulipoanza CAR mwezi Oktoba mwaka jana kama inavyoonekana kwenye shule hii mjini Bangui. (Picha:MINUSCA)

Shule nyingi CAR bado zimefungwa:UNICEF

Ikiwa muhula wa kwanza wa masomo umefikia ukingoni huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, bado shule nyingi zimefungwa hali inayotia wasiwasi shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na pande mbili hizo umebaini kuwa tangu muhula wa kwanza uanze mwezi Oktoba mwaka jana, shule zilifunguliwa kwa wastani wa wiki nne tu kutokana na uharibifu wa majengo, walimu kutokuwepo shuleni na hata kuchelewa kwa mishahara ya walimu.

Souleymane Diabaté ambaye ni mwakilishi mkazi wa UNICEF nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema wamegundua pia theluthi moja ya shule 355 zilizopitiwa na utafiti huo zimekumbwa na mashambulizi miezi ya karibuni pamoja na vifaa kuporwa.

Jambo lingine ni kwamba utoro umeripotiwa kwa kiasi kikubwa ambapo mtoto mmoja kati ya watatu walioandikishwa shule mwaka jana, hawakurejea shule mwaka huu.

Mwakilishi huyo wa UNICEF amesema kinachoonekana sasa ni kwamba mfumo wa elimu Jamhuri ya Afrika ya Kati umeanguka, walimu hawajalipwa mishahara, hakuna vitabu vya kiada na hata miundombinu ya shule iliyokuwepo kabla ya mzozo sasa imeharibiwa.

Kwa sasa UNICEF inasaidia serikali kupata vifaa vya shule maeneo ambako vimeporwa ili watoto waweze kurejea shuleni na imesihi usaidizi zaidi wa fedha kwani mpango wake wa elimu umepata dola Milioni Tatu tu kati ya Milioni 10 zinazohitajika kusaidia watoto warejee shuleni.