Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay arejelea wito wake kwa suala la Syria kuwasilishwa ICC

Pillay arejelea wito wake kwa suala la Syria kuwasilishwa ICC

Nimerejelea wito wangu kwa Baraza la Usalama kuwasilisha suala la Syria kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay akirejelea wito wake wa kwanza wa aina hiyo mwezi Agosti mwaka 2011.

Pillay amesema hayo kwa waandishi wa habari baada ya kuhutubia baraza la usalama kwenye kikao cha faragha kuhusu hali ilivyo huko Syria, Jamhuri ya Afrika, Sudan Kusini, Mali na Libya.

Amesema tangu atoe wito wa aina hiyo ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na vikosi vya serikali na vile vya upinzani unaendelea na lazima haki itendeke.

(Sauti ya Pillay)

"Wakati wanachama wengi wanasisitiza wazo la suluhu la kisiasa kama ilivyo kwa katibu mkuu wakati huu ambapo mazungumzo yanaendelea, ni lazima kuwepo na haki na uwajibikaji na hali inayoendelea Syria haipaswi kutoweka hivi hivi.”

Alipoulizwa kuhusu Jamhuri ya Afrika ya Kati, Pillay amesema suala hilo limejadiliwa kwa kina kwenye mashauriano ya faragha wakati huu ambapo ghasia zinazosababishwa na kikundi kilichojihami cha Anti-Balaka kimesababisha karibu asilimia 80 ya waislamu kukimbia makazi yao. Hivyo akasema..

(Sauti ya Pillay)

Nafikiri kuna umuhimu wa kuimarisha kikosi! Natumaini baraza la usalama litaendelea na mpango wa kuanzisha ujumbe wa kulinda amani nchini humo. Katika vijiji vyote tulivyoenda wametuambia wanataka polisi kwa usalama wao. Kwa hiyo iwapo ujumbe huo wa kulinda amani utajumuisha polisi Elfu Mbili kama alivyopendekeza Katibu Mkuu, hiyo itakuwa msaada wa haraka sana kwa wananchi.”