Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaunga mkono SCHOLAS, mpango wa Papa Francis kuhusu barubaru

UNICEF yaunga mkono SCHOLAS, mpango wa Papa Francis kuhusu barubaru

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF imeingia ubia na mpango ulioanzishwa na kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis wa kusaidia vijana barubaru duniani, SCHOLAS.

Tangazo la ubia huo limekuja wakati Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake alipokutana na na Papa Franscis huko Vatican, ambapo SCHOLAS inalenga kusaidia barubaru wa kike na wa kiume kupata stadi zaidi, taarifa na uelewa wa kile wanachohitaji ili kuchangia katika maendeleo siyo jamii zao tu bali dunia nzima kwa ujumla.

Bwana Lake amesema ushirikiano huo wa miaka mitano unazingatia mambo ambayo Vatican na UNICEF wanaamini kuhusu uthabiti wa vijana ambapo vijana wasio na fursa zaidi watawezeshwa kukutana pamoja kupitia michezo, sanaa na teknolojia na kutambuana na kubadilishana mawazo.

Kwa kuanzia UNICEF na SCHOLAS watashirikiana katika shughuli za kimataifa zinazoshikisha vijana mathalani kusaidia kutokomeza ghasia, kuendeleza ushirikiano baina ya vijana na kuwakutanisha.