Mbinu mbadala zahitajika kupatia suluhu tatizo la maji duniani:

27 Oktoba 2013

Licha ya kwamba maji ni haki ya msingi, bado mamilioni  ya watu wanakosa huduma hiyo na hata wengine pale wanapoipata inakuwa ni bei ya juu na usalama wake ni mashakani. Amesema Peter Gleick wa taasisi ya Pacific ya Californian chini Marekani alipohojiwa na shirika la fedha duniani, IMF  juu ya hatma ya rasilimali hiyo adhimu.

Gleick amesema uhaba wa maji unazidi kuibua migogoro kati ya nchi na nchi na hata ndani ya nchi baina ya jamii za wakulima na wafugaji na kusema mbinu za karne ya 20 za kutegemea maji yamito, kuchimba mabwawa zimepitwa na wakati.

(Sauti ya Gleick)

Ni lazima tufikirie upya upatikanaji wa maji kutoka vyanzo kama vile kutakasa majitaka, uvunaji maji ya mvua, kutumia maji ya ardhi tena na tena badala ya kuchukua maji kutoka vyanzo ambavyo tayari vimezidiwa uwezo kama vile mito na maziwa. Pili tuangalie upya  mahitaji: Tunaweza kutumia maji kidogo zaidi kuliko vile tunavyotumia sasa mathalani kwenye  umwagiliaji: hayo ndio matumizi ya tija ya maji. Na tatu ni kuweka mfumo wa kiuchumi stahili wa maji: tuweke mfumo bora wa bei ambao unajali jamii maskini.’

Gleick ametaja pendekezo lingine kuwa ni kujumuisha taasisi zinazohusika na masuala ya maji ili ziweze kushughulikia suala la maji kwa pamoja kwa kuzingatia matumizi yenye tija, mabadiliko ya tabia nchi na hata vyanzo vipya.