Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

UM wakumbusha 'walio vizuizini wana haki za kiutu na lazima zihishimiwe'

Kamisheni ya UM juu ya Haki za Binadamu imeanzisha kampeni maalumu ya kimataifa itakayoendelezwa hadi Oktoba 12 (2008) ambapo taasisi za kizalendo zinazogombania haki za binadamu katika nchi wanachama wa UM, pamoja na mashirika yasio ya kiserikali na wadau wengine husika zitajumuika kukumbushana juu ya ulazima, na umuhimu, wa kuhakikisha watu waliowekwa vizuizini na kwenye magereza huwa wanatekelezewa haki zao zote halali za kimsingi.

Mkuu wa UNHCR atetea haki za mafakiri na wahamaji waliokosa makazi ulimwenguni

António Guterres Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Wahamiaji (UNHCR) kwenye risala ya ufunguzi mbele ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa mwaka Geneva wa Kamati ya Utendaji ya UNHCR, ya kwamba maslahi ya watu mafukara na wale waliong’olewa makwao ulimwenguni yamo hatarini sasa hivi, kwa sababu ya mchanganyiko wa athari mbalimbali zinazochochewa na migogoro iliofumka karibuni ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hali ambayo, alisema anakhofia itazusha watu kungo’lewa zaidi makazi katika miaka ijayo.

Siku ya Makazi Bora 2008

Shirika la UM juu ya Makazi (UN-HABITAT) kila mwaka huiadhimisha Ijumatatu ya mwanzo wa mwezi Oktoba kuwa ni Siku ya Makazi Bora Duniani. Lengo la taadhima hizi ni kutathminia hali ya miji na haki za kimsingi za mwanadamu kupatiwa makazi ya kiutu kwa wote, pamoja na jukumu la jamii ya kimataifa katika kuyatekeleza hayo.

Hapa na Pale

Alain Le Roy, Naibu KM mpya wa Idara yaUM kuhusu Operesheni za Ulinzi Amani Duniani (DPKO) amewasili Sudan Ijumatatu asubuhi, kwa ziara ya wiki moja. Dhamira ya ziara hii ni kujijulisha na kukutana kwa mashauriano na viongozi wa Serikali ya Muungano wa Taifa na Serikali ya Sudan Kusini, pamoja na washiriki wengine wa huduma za amani wa eneo hilo la Afrika. Kadhalika Le Roy anatazamiwa kukutana na wakuu wa mashirika ya amani ya UM katika Sudan ya UNMIS, na wakuu wa vikosi vya amani vya mchanganyiko vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa Darfur, UNAMID. Le Roy alianza madaraka mapya ya khatamu za kuendesha Idara ya DPKO mwezi Agosti mwaka huu.

Hali Usomali inatia wasiwasi: OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura na Huduma za Kiutu (OCHA) imeripoti mnamo wiki hii, raia karibu 80 waliuawa na zaidi ya watu 100 walijeruhiwa baada ya vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika (UNISOM) viliposhambuliwa kwenye mji wa Mogadishu na makundi yanayopinga serikali.

IOM itapanua huduma za kuokoa watoto waliotoroshwa Afrika Magharibi

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limetangaza leo kwamba litapanua zaidi mradi wa kusaidia kurejesha makwao wale watoto waliotekwa nyara Afrika Magharibi, na ambao hushirikishwa kwenye kazi za kulazimisha katika nchi za kigeni. Mradi huu ulianzishwa mwaka 2006, na unafadhiliwa na Idara ya Masuala ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kamati ya Kwanza ya BK imepitisha ajenda ya kikao cha 63

Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu (BK), inayohusika na Masuala ya Usalama wa Kimataifa na Upunguzaji wa Silaha imepitisha ajenda na ratiba ya kikazi kuzingatiwa kwenye kikao cha safari hii cha 63, ikijumlisha suala la kuzuia mashindano ya silaha nje ya dunia, na kukomesha biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, pamoja na suala la kujikinga na hatari ya magaidi kupata silaha za maangamizi ya halaiki.~

Kamati ya Nne imeafikiana kusailia amani, ukoloni na masuala maalumu ya kisiasa

Kamati ya Nne ya Baraza Kuu inayozingatia Masuala Maalumu ya Kisiasa na Kuondosha Ukoloni ilikutana kwenye mkutano mfupi Alkhamisi, na ilipitisha ajenda ya kusailiwa kwenye kikao cha mwaka huu, ambapo zaidi ya mada 12 zitajadiliwa, zikijumuisha vie vile masuala juu ya matumizi ya amani ya sayari nyengine, nje ya dunia, operesheni za ulinzi amani za UM na uondoshaji wa ukoloni kwenye Maeneo Yasiojitawala. ~