Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala wa mwaka wa BK umemalizika na Raisi wake ahamasisha mabadiliko ya kidemokrasia katika UM

Mjadala wa mwaka wa BK umemalizika na Raisi wake ahamasisha mabadiliko ya kidemokrasia katika UM

Kwa muda wa karibu wiki mbili hivi, Wakuu wa Taifa na Serikali 111 walisimama mbele ya wajumbe wa kimataifa, kwenye ukumbi wa Baraza Kuu kuelezea wasiwasi walionao juu ya masuala kadha muhimu ambayo wangelipendelea kuona yanapewa usikivu mzuri zaidi na jumuiya ya kimataifa.

Hivi sasa mijadala ya Baraza Kuu ya wawakilishi wote imeshamalizika, na kuanzia Ijumatatu, ya tarehe 06 Oktoba kamati sita za Baraza Kuu zitakusanyika kusailia masuala maalumu mbalimbali yanayoambatana na ajenda iliopitishwa kwenye Baraza hilo. Rsisi wa Baraza Kuu, Miguel d’Escoto kwenye hotuba yake ya kufunga mjadala wa wawikilishi wote, mapema wiki hii, aliwakumbusha tena wajumbe wa kimataifa kwamba wanakutana katika kipindi ambapo alikitafisiri kama “kipindi cha mfumo wa uchumi wa kimataifa uliojaa dosari, na unaokaribia kuporomoka”. Hali hiyo, alitilia mkazo, ni lazima irekibishwe na shughuli za kikazi zisiruhusiwe tena kuendelea kama kawaida kwa sababu zifuatazo:

"Sote tunatambua uzito mkuu wa mzozo huu, ambao mizizi yake inatokana na kichaa cha uchoyo na ubinafsi, hali ambayo ndiyo inayotawala utamaduni wa siku hizi unaoshikilia kusema kila kitu ni miye na kila kitu ni changu. Lakini kinachonitia moyo kutokana na majadiliano ya jumla ya mwaka huu ni kuona fungu kubwa la wajumbe wa kimataifa walizungumzia juu ya matatizo yanayotuhusu sisi na yalio yetu pamoja. Wawakilishi wanaopendelea ujasiri wa hali ya juu na huruma za kibinadamu nimeona idadi yao imezidi sana ile ya wale wajumbe wakakamavu wa mataifa yenye kuhamasisha hofu, woga na hali ya kutoaminiana miongoni nchi wanachama."

Raisi wa Baraza Kuu d‘Escoto alikumbusha vile vile mkorogano wa fedha uliojiri sasa hivi katika soko la kimataifa ulidhihirika wazi kabisa pale mgogoro wa chakula ulipofumka:

"Inastaajabisha kwamba baada ya miaka 63 sisi wanadamu bado tunakabiliwa na ule ukweli, uliofurika aibu na fedheha, ya kuwa mamia milioni ya umma wa kimataifa unateseka na kusumbuliwa vibaya na matatizo ya njaa na utapiamlo uliohanikiza kwenye majira yaliojaa neema. Hiki, kusema kweli ni kichaa kisiosameheka, na hali yenye kuonyesha dhahiri songombingo ya mawazo yaliokosa uamuzi wa kutambua masuala gani yanafaa kuepewa umuhimu kwa natija ya umma wa kimataifa."

Katika kufunga risala yake Raisi wa Baraza Kuu Miguel d’Escoto alisema tuna deni kumlipa 'Mama Dunia' ambaye anajitahidi kujivua na madhara yalioletwa kwenye mazingira yake kufuatia matumizi mabaya ya wanadamu. Alisema tuna deni kuu kwa vizazi vijavyo, waliopo pembe zote za dunia, jukumu ambalo linatuwajibisha kuhakikisha tunakabili matatizo ya kimataifa, kwa pamoja na tuweke kando tofauti zetu ndogo ndogo zenye kusababisha mivutano isio maana. Alisema mabadiliko yenye natija kwa wanadamu wote yanaweza kuwasilishwa kwa ushirikiano wa pamoja katika miezi ijayo dhidi ya madhara yenye kuhatarisha usalama na amani ya kimataifa.

Kuanzia wiki ijayo Baraza Kuu litaendeleza vikao kadha wa kadha kuzingatia ajenda ya kikao cha 63, mikutano itakayoendelea hadi wiki za mwisho za Disemba ambapo miongoni mwa mambo yatakayosailiwa ni pamoja na masuala yanayohusu taratibu za kuleta marekibisho na mageuzi ya kidemokrasia katika UM yenyewe, na pia mada juu ya ufadhili wa miradi ya maendeleo, na kadhalika udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye ulimwengu uliogawanyika na wenye fungamano kubwa za kiikolojia.