Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na pale

Ijumatano, KM Mdogo na Mshauri wa UM juu ya Misaada ya Daharura, John Holmes alikamilisha ziara ya siku tatu Ethiopia. Ijumanne, Holmes alizuru eneo la wenyeji wa asli ya Kisomali, sehemu ya nchi iliodhurika sana na ukame, pamoja na bei kubwa ya chakula na mgogoro unaozidi kuendelea katika eneo lao. Kwenye kituo cha ukaguzi juu ya hadhi za wahamiaji, Holmes akikutana na wenyeji raia wa Kisomali na Kiethiopia waliokata tama ya maisha na ambao walitaka kusaidiwa kihali, halan. Alikumbusha Holmes ya kuwa ukosefu wa misaada ya kiutu umewalazimisha wahamiaji wingi wa Kiethiopia kutafuta hifadhi ya kisiasa, kwa matumaini ya kupatiwa chakula, makazi na huduma za afya.

Ubashiri wa hali ya hewa ni muhimu kupunguza umasikini na kutunza rasilimali ya maji

Michel Jarraud, Mkurugenzi wa Shirika la UM juu ya Upimaji wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) aliwaambia wawakilishi waliohudhuria Mkutano wa Dunia juu ya Maji unaofanyika kwenye mji wa Montpellier, Ufaransa kwamba ni muhimu kwa nchi wanachama kutumia ujuzi wa kisasa wa kutabiri hali ya hewa wakati wanapoandaa miradi ya maendeleo ya uchumi na kupunguza umaskini unaochochewa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa, hususan wanapotathminia akiba ya maji.

Ndege ya kuhudumia misaada ya dharura katika JKK imeanguka

Ndege iliokodiwa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) kuhudumia misaada ya kiutu katika JKK iliripotiwa alasiri ya Ijumatatu ilijigonga na mlima, kilomita 15 kaskazini-mashariki ya Uwanja wa Ndege wa Bukavu wakati ilipokuwa ikielekea huko kutokea Kinshasa na ikichukua abiria 15 pamoja na marubani wawili, kwa mujibu wa taarifa za mwanzo tulizopokea kutoka msemaji wa OCHA Kinshasa, Christopher Illemassene.

UNEP imenasihi ajali zisokwisha za kimaumbile zaweza kukomeshwa panapo udhibiti bora wa hali ya hewa

Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) leo ametoa taarifa iliohadharisha kwamba pindi mabadiliko ya hali ya hewa yatashindwa kudhibitiwa kama inavyostahiki kisayansi, kuna hatari ya maaafa ya kimaumbile kukithiri na kuathiri kihali na mali umma wa kimataifa, kama ilivyotukia wiki hii katika mji wa New Orleans, Marekani ambapo Kimbunga Gustav kilisababisha maelfu ya watu kuhamishwa makwao na kupelekwa kwenye maeneo salama.

Hapa na Pale

Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Septemba atakuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Burkina Faso ambaye atawasilisha ajenda ya mwezi ya shughuli za Baraza Ijumatano.

Taarifa fupi za habari kwa Ijumatatu[Ofisi za UM Makao Makuu zilifungwa 01/09/2008]

Ijumatatu, Septemba mosi Jaji Navanethem Pillay ameanza rasmi madaraka mapya ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) ambapo ataongoza taasisi inayoendelea kukua yenye watumishi 1,000 wanaohudumia utekelezaji wa haki za binadamu katika nchi 50 ulimwenguni. Bi Pillay ni mwanasheria wa kutoka Afrika Kusini ambaye mwezi Julai aliteuliwa kuongoza ofisi ya UM juu ya haki za binadamu, kufuatia pendekezo la KM Ban Ki-moon. Tangu 2003, Jaji Pillay alitumikia Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) iliopo Hague, Uholanzi – mahakama ya kwanza huru, ya kudumu, iliobuniwa na jumuiya ya kimatraifa kushughulikia kesi zinazohusu mauaji ya kuangamiza halaiki ya watu, makosa ya vita na jinai dhidi ya utu. Kabla ya hapo Pillay alikuwa Jaji na pia Raisi wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) ambayo alijiunga nayo kuanzia 1995.