Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa fupi za habari kwa Ijumatatu[Ofisi za UM Makao Makuu zilifungwa 01/09/2008]

Taarifa fupi za habari kwa Ijumatatu[Ofisi za UM Makao Makuu zilifungwa 01/09/2008]

Ijumatatu, Septemba mosi Jaji Navanethem Pillay ameanza rasmi madaraka mapya ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) ambapo ataongoza taasisi inayoendelea kukua yenye watumishi 1,000 wanaohudumia utekelezaji wa haki za binadamu katika nchi 50 ulimwenguni. Bi Pillay ni mwanasheria wa kutoka Afrika Kusini ambaye mwezi Julai aliteuliwa kuongoza ofisi ya UM juu ya haki za binadamu, kufuatia pendekezo la KM Ban Ki-moon. Tangu 2003, Jaji Pillay alitumikia Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) iliopo Hague, Uholanzi – mahakama ya kwanza huru, ya kudumu, iliobuniwa na jumuiya ya kimatraifa kushughulikia kesi zinazohusu mauaji ya kuangamiza halaiki ya watu, makosa ya vita na jinai dhidi ya utu. Kabla ya hapo Pillay alikuwa Jaji na pia Raisi wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) ambayo alijiunga nayo kuanzia 1995.

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK na kiongozi wa Shirika la UM juu ya Ulinzi wa amani katika JKK (MONUC) ametoa taarifa yenye kuthibitisha hali ya shwari imerejea Rutshuru, ile sehemu iliopo kwenye jimbo la vuguvugu na vurugu la Kivu Kaskazini kufuatilia mapambano baina ya vikosi vya Serikali na makundi ya waasi yaliokuwa na silaha. Ijumapili, Doss, akifuatana na Waziri wa Ulinzi wa JKK, Tshikez Diemu walizuru eneo kwa kutathminia hali halisi ya usalama baada ya mapigano kusita. Vikosi vya jeshi la taifa vya FARDC vilishiriki kwenye mapigano hayo na kundi la waasi la CNDP, mapigano ambayo yanasemekana yalikuwa ni mabaya zaidi tangu mwafaka wa kurudisha usalama ulipotiwa sahihi na makundi husika mwezi Januari. MONUC imetoa mwito kwa makundi yote hayo yanayohasimiana kujizuia na mapigano, kurejea kwenye maeneo waliokuwepo kabla ya mapambano na papo hapo kujiepusha na vitendo vyote vya uchokozi, na MONUC imeshatuma vikosi maalumu vya doria kwenye eneo kuimarisha usalama.

Ijumatatu kwenye ofisi za UM Geneva kulifanyika taadhima maalumu za kumbukumbu ya msiba wa tarehe 19 Agosti 2003, ambapo makao makuu ya ofisi za UM mjini Baghdad ziliposhambuliwa na bomu liliosababisha vifo vya wafanyakazi wa UM 22 na kujeruhi zaidi ya watu 150 wengineo. KM Ban Ki-moon kwenye risala yake mbele ya aila za waathiriwa wa ajali hiyo, pamoja na wale walionusuruika kifo, alisema ameamua, kwa nia thabiti, kwamba "UM utafanya kila iwezalo kuhakikisha msiba kama ule uliotukia kwenye ofisi zake za Baghdad hautorudiwa tena!” Alisema UM utaendeleea kuusaidia umma wa Iraq kuwasilisha amani na maendeleo katika taifa lao. Aliongeza kusema kwamba UM sasa hivi unaandaa mradi maalumu wa kujenga majengo mapya makubwa kwa watumishi wa UM Iraq, majengo ambayo yatazatitiwa ulinzi kama ngome ili kuhakikisha watumishi wa kimataifa wanapata hifadhi wanaostahiki. Kadhalika UM unajaribu kuyatekeleza mapendekezo ya karibuni ya ile tume huru juu ya usalama na ulinzi wa majengo na ofisi za UM katika ulimwengu, tume ambayo iliundwa Disemba 2007 kufuatilia shambulio la bomu la ofisi za UM katika mji wa Algiers, Algeria ambapo watumishi 19 wa UM waliuawa.