Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndege ya kuhudumia misaada ya dharura katika JKK imeanguka

Ndege ya kuhudumia misaada ya dharura katika JKK imeanguka

Ndege iliokodiwa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) kuhudumia misaada ya kiutu katika JKK iliripotiwa alasiri ya Ijumatatu ilijigonga na mlima, kilomita 15 kaskazini-mashariki ya Uwanja wa Ndege wa Bukavu wakati ilipokuwa ikielekea huko kutokea Kinshasa na ikichukua abiria 15 pamoja na marubani wawili, kwa mujibu wa taarifa za mwanzo tulizopokea kutoka msemaji wa OCHA Kinshasa, Christopher Illemassene.

Kampuni ya ndege ya binafsi, inayoitwa Aid Serv, yenye makao yake Marekani ndio yenye kumiliki ndege hiyo. Katika taarifa iliotolewa na kampuni kwa waandishi habari ilisema kwamba "hakuna dalili ya abiria kunusurika na ajali hiyo". Mabaki ya ndege yaligunduliwa leo kwa helikopta baada ya kupokea taarifa kwamba ndege ilipotea.

KM Ban Ki-moon ameripotiwa, kwa kupitia msemaji wake, kuwa alihuzunishwa sana na ajali ya ndege katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK). Alisema anajumuika na jamaa za washiriki wenzi kuomboleza na kuwakumbuka wafanyakazi wa UM na watumishi wa mashirika yasio ya kiserikali, pamoja na maofisa wa Kongo na marubani wa ndege, waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo. Aliwashukuru watumishi wote wa UM na pia wahudumia misaada ya kiutu wa kimataifa waliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) ambao wanaendelea kufanya kazi zao bila uchofu, kwenye mazingira magumu, kwa lengo la kuusaidia umma na raia wa Kongo kuimarisha usalama na amani ya taifa lao.

Sikiliza taarifa kamili kwenye idhaa ya mtandao.