Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

KM akutana na wawakilishi wa ASEAN kuzingatia Myanmar

KM Ban Ki-moon alimaliza mashauriano muhimu Ijumatano usiku na wawakilishi wa kutoka Mataifa Wanachama wa Umoja wa ASEAN, walio jirani na Myanmar, na vile vile kujumuisha wawakilishi wa yale mataifa wafadhili kuzingatia hali katika Myanmar na kuzingatia hatua za kuchukuliwa, kidharura, kuharakisha misaada maridhawa inayotakikana kunusuru maisha ya umma ulioathirika na Kimbunga Nargis katika Myanmar. Wajumbe hawa waliafikiana kuitisha kikao maalumu mwezi ujao cha kuchangisha msaada unaotakikana kuihudumia Myanmar kufufua tena shughuli zake za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya umma, kwa ujumla.

Bei za chakula ziliteremka Aprili, yaripoti FAO

Viashirio vya bei za chakula vinavyotayarishwa na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) vimethibitisha kwamba katika mwezi Aprili bei ya baadhi ya vyakula iliteremka, kwa mara ya kwanza, baada ya miezi 15 ya mifumko ya bei za chakula zilizokuwa zikipanda bila kikomo. Vyakula vilivyosajiliwa kuteremka bei kwa kiwango cha 0.3 vilijumuisha ngano, sukari, bidhaa za maziwa na maharagwe ya soya.~

Mukhtasari wa kikao cha 61 cha Baraza la Utendaji la WHO

Kikao cha 61 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani (WHO) kinatarajiwa kujumuika mjini Geneva, Uswiss kuanzia tarehe 19 mpaka 24 Mei 2008 ambapo masuala muhimu yanayohusu udhibiti bora wa matatizo ya afya ya kimataifa yatazingatiwa. Wajumbe wa kutoka Mataifa Wanachama 193 wanatazamiwa kuhudhuria kikao hiki cha mwaka.

BU kulaumu mashambulio ya JEM dhidi ya Serikali Sudan

Ijumanne Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Mei, Balozi John Sawers wa Uingereza aliwaarifu waandishi habari kwamba wajumbe wa Baraza wamekubaliana kushtumu vikali, kwa kauli moja mashambulio ya silaha dhidi ya Serikali yalioendelezwa na wafuasi wa kundi la waasi wa Darfur la JEM katika tarehe 10 Mei kwenye eneo la Omdurman, kitongoji kilichopo nje ya mji mkuu wa Khartoum, Sudan.

UM unaendelea na operesheni za dharura katika Myanmar

Mashirika kadha ya UM bado yanaendelea kuhudumia misaada ya kiutu kwa umma wa Myanmar ulioathirika na Kimbunga Nargis, tufani ambayo iligharikisha sehemu kadha za taifa hilo katika siku kumi zilizopita. Hivi sasa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeshakamilisha misafara ya kupeleka Myanmar tani za metriki 360 ziada za chakula zitakazosaidia kuwahudumia lishe bora waathiriwa 750,000 mnamo miezi 3 ijayo. ~~