Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Dokezo ya ripoti ya OHCHR juu ya vurugu Kenya baada ya uchaguzi

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) Ijumatano imetoa ripoti yenye kuelezea matokeo ya ziara ya wiki tatu Kenya, iliofanywa na wataalamu mwezi uliopita ambapo walichunguza kiini halisi cha machafuko na vurugu liliolivaa taifa hilo kufuatia uchaguzi wa Raisi katika Disemba 27, 2007.~

Mazungumzo ya Sahara Magharibi yamekhitimisha duru ya nne mjini New York

Duru ya nne ya mazungumzo ya siku mbili kuzingatia suala la Sahara ya Magharibi imemaliza mijadala yake Ijumanne katika wilaya ya Manhasset, kwenye jimbo la New York. Vikao viliongozwa na Mjumbe wa KM kwa Sahara ya Magharibi, Peter van Walsum, na kuhudhuriwa na wawakilishi wa Morocco, Chama cha Ukombozi cha Frente Polisario pamoja na wajumbe kutoka mataifa jirani ya Algeria na Mauritania.

Baadhi ya wajumbe wa BU hawakufurahika na juhudi za upatanishi Myanmar

Baadhi ya mabalozi wa nchi wanachama katika Baraza la Usalama (BU) wamenakiliwa kuonyesha kuwa na masikitiko makubwa juu ya mzoroto wa zile juhudi za karibuni za upatanishi katika Myanmar zilizoongozwa na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar, Ibrahim Gambari. Lakini hata hivyo, wajumbe hawa waliahidi kwamba wataendelea kulimurika suala la Myanmar kwenye mijadala yao ili kuhakikisha linapatiwa suluhu ya kuridhisha na ya haki yenye masilahi kwa umma.

Arbour kuyahimiza mataifa yaridhie Mkataba wa Kuondosha Ubaguzi Duniani

Louise Arbour, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu Duniani ametoa mwito maalumu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kufyeka Ubaguzi, mwito ambao umependekeza kwa Mataifa Wanachama kuidhinisha haraka ule Mkataba wa Kimataifa wa 1969 wa Kuondosha Aina Zote za Ubaguzi Ulimwenguni, na kujitahidi kuimarisha sheria zao kitaifa ili kuhakikisha waathiriwa wa janga la ubaguzi huwa wanapatiwa haki. Siku ya Kimataifa Kuondosha Ubaguzi huadhimishwa kila mwaka na jamii ya UM katika tarehe 21 Machi.~

WHO inahimiza kuongezwe juhudi za kupambana na TB Duniani

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa ripoti mpya yenye mada isemayo Udhibiti wa Maradhi ya Kifua Kikuu (TB) Duniani 2008. Ripoti ilibainisha ya kuwa watu milioni 9.2 walipatwa na maradhi ya kifua kikuu katika 2006, idadi ambayo ilijumuisha, vile vile, watu 700,000 waliokuwa na virusi vya UKIMWI, pamoja na watu 500,000 ziada walioelemewa na kuugua TB sugu inayokataa hata ile tiba maarufu ya madawa ya mchanganyiko.~~

Vurugu la machafuko Kenya latathminiwa na Baraza la Haki za Binadamu

Francis Deng, Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu juu ya Uzuiaji wa Mauaji ya Halaiki aliyewasilisha ripoti maalumu Ijumatatu mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva iliotathminia shughuli za ofisi yake. Deng alisailia juu ya juhudi za jumuiya ya kimataifa za kuhakikisha migogoro ikizuka kutachukuliwa hatua za dharura kuidhibiti mizozo hiyo mapema, na pia kujaribu kubashiria udhibiti bora wa dalili zote ambazo huenda zikachochea maangamizi ya halaiki. Kwenye ripoti Deng alitoa mfano namna mapendekezo haya yalivyotekelezwa nchini karibuni, kufuatia matokeo ya uchaguzi mnamo mwisho wa mwaka uliopita.

Bukini imetia sahihi ya kuridhia Mkataba wa Roma

Mapema wiki hii taifa la Bukini limetia sahihi ya kuridhia Mkataba wa Roma, ambao ndio ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya ICC. Mahakama ya ICC ni mahakama huru na ya kudumu, iliyodhaminiwa na jumuiya ya kimataifa madaraka ya kuhukumu wale watu waliotuhumiwa kufanya makosa mabaya ya jinai, mathalan, mauaji ya halaiki, jinai ya vita na vile vile yale makosa ya uhalifu dhidi ya utu.