Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

WFP imeanza kugawa chakula Bukini kwa waathiriwa wa Tufani Ivan

Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeanzisha huduma za dharura za kugawa chakula katika yale maeneo ya Bukini yaliodhirika na uharibifu wa Tufani Ivan iliopiga wiki iliopita. Makumi elfu ya watu wanategemea misaada hiyo ya kihali kutoka mashirika ya UM, hususan ule umma unaoishi kwenye mahema mjini Antananarivo, ambao nyumba zao ziliharibiwa na tufani, pamoja na wale watu wanaoishi kwenye sehemu za mwambao wa mashariki ya Bukini na kwenye kisiwa cha St. Marie, maeneo yalioumia zaidi na gharika ya Tufani Ivan.

Juhudi za kupunguza umaskini Tanzania kwa kutumia nishati mbadala (Sehemu ya Pili)

Katika makala iliopita, tulikupatieni sehemu ya kwanza ya mazungumzo na Bariki Kaale, mtaalamu wa nishati katika ofisi ya Dar es Salaam ya Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Miradi ya Maendeleo Duniani (UNDP). Alisaiilia juhudi za wanavijiji kutumia kile alichokiita “nishati endelevu” iliyo rahisi, ambayo umma wa kawaida wataimudu na itawasaidia kukuza maendeleo yao kwa ujumla.

UNICEF yajitolea kufufua elimu ya msingi Liberia

Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF), ambaye anazuru Liberia wiki hii, ametangaza kufadhilia taifa hilo msaada wa dola milioni 20 zitakazotumiwa kufufua tena sekta ya ilmu ya msingi, ambayo iliharibiwa na vile vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoshtadi nchini humo kwa muda wa miaka kumi na tano.

Raia wa Chad waliokimbilia Cameroon wahamishwa tena kwenye kambi mpya

Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti wahamiaji 5,500 waliokimbia mapigano mwanzo wa mwezi kutoka mji wa N’Djamena, Chad na ambao walikuwa wakiishi kwenye makazi ya muda kaskazini-mashariki ya Cameroon, hivi sasa wamepelekwa uhamishoni kwenye kambi mpya ziliopo kijiji cha Maltam, kitendo ambacho kinatazamiwa kurahisisha ugawaji wa misaada ya kihali kwa umma husika kutoka mashirika ya kimataifa.Kadhalika uhamisho huu utayawezesha mashirika yanayohusika na misaaada ya kiutu kuwapatia wahamiaji hawo hifadhi kinga. Jumla ya wahamiaji 30,000 wa Chad hivi sasa wanaishi kwenye maskani ya muda katika eneo la Cameroon kaskazini.

Khofu ya kurejea makwao inawasumbua Wakenya waliokimbilia Uganda

UNHCR imeripoti kwamba asilimia kubwa ya raia 12,000 wa Kenya waliovuka mpaka na kwenda Uganda kupata hifadhi, baada ya machafuko kuzuka nchini kufuatia uchaguzi wa Disemba 27 mwaka jana, kuwa wanakhofu kurejea makwao kwa hivi sasa, licha ya kuwa ripoti za jamii ya kimataifa zilithibitisha hali ya usalama, kwa ujumla, nchini imeanza kutengenea.

KM ahimiza maendeleo ya haraka Kenya kwenye mazungumzo ya upatanishi

Msemaji wa Katibu Mkuu, Michele Montas amearifu kwenye mkutano wa hadhara ya kwamba Katibu Mkuu Ban Ki-moon ametoa risala yenye kuhimiza yale makundi yanayohusika na Mazungumzo ya Taifa na Upatanishi Kenya, kufanya kila wawezalo, na kuchukua hatua za haraka, kuhakikisha watafikia suluhu ya kuridhisha juu ya mfarakano uliolivaa taifa lao.

Eritrea imekakamaa kuiwekea UNMEE vikwazo

Shirika la Ulinzi wa Amani Mipakani Ethiopia/Eritrea (UNMEE) limearifu kwamba wanajeshi wa Eritrea bado wanaendelea kuwaekea vikwazo dhidi ya shughuli zake. UNMEE ilitoa mfano wa kitendo kilichotukia juzi ambapo magari 8 ya UM yalizuiliwa kuelekea mji wa Asmara kukusanya vifaa vya uhamisho wa muda vya watumishi wa UNMEE waliotarajiwa kupelekwa taifa jirani la Ethiopia.

'Twachoka kusubiri', unyanyasaji wa wanawake ukomeshwe halan - KM Ban

KM Ban Ki-moon Ijumatatu alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri kadha walioshiriki kwenye taadhima za ufunguzi rasmi wa kikao cha mwaka cha 52 cha Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake (CSW). Kwenye risala ya ufunguzi, mbele ya wawakilishi wa kimataifa, KM Ban alichukua fursa ya kuanzisha kampeni ya kimataifa itakayojumuisha UM na mashirika yake yaliozagaa kote duniani, na kuchangisha serikali za Nchi Wanachama na jumuiya za kiraia, halkadhalika, kufyeka kidharura, na kwa nguvu moja, vitendo vyote vya unyanyasaji, utumiaji mabavu na udhalilishaji wa wanawake. Alisema vitendo karaha kama hivi dhidi ya wanawake havistahamiliki kamwe. ~~Sikiliza taarifa kamili kwenye idhaa ya mtandao.