Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya raia CAR wakimbilia vichakani na kunyimwa mahitaji ya kimsingi

Maelfu ya raia CAR wakimbilia vichakani na kunyimwa mahitaji ya kimsingi

Toby Lanzer, Mshauri wa Umoja wa Mataifa juu ya Misaada ya Dharura kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwenye mkutano na waandishi habari katika Makao Makuu ya UM alibainisha kwamba mashirika ya UM yanakabiliwa na tatizo gumu la kuhudumia misaada ya kiutu fungu kubwa la wahamiaji wa ndani ya nchi 200,000 waliokimbilia vichakani kaskazini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). Wahamiaji hawa huwa wanakimbilia vichakani kuwakwepa majambazi wenye silaha ambao hushambulia raia kihorera.

Wafanyakazi wa mashirika ya UM wanaohudumia misaada ya kiutu wameshindwa hivi sasa kuwapelekea umma huo misaada ya kukidhi mahitaji yao ya kimsingi, mathalan, maji safi, huduma za utunzaji afya, mbegu na vifaa vya kulimia. Kadhalika UM haukafanikiwa kuendeleza masomo ya msingi kwa watoto 75,000 ambao, pakiwepo utulivu wa kawaida huwa wanahudhuria madarasa kwenye zile skuli za mabanda ya nyasi.