Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila uwakili wenu malengo ya SDG’s hayatofanikiwa:Guterres

Bila uwakili wenu malengo ya SDG’s hayatofanikiwa:Guterres

Pakua

Tunatambua kwamba utandawazi na maendeleo ya teknolojia vimeleta faida kubwa duniani , lakini watu wengi bado wamesalia nyuma.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antinio Guterres leo alipokutana na mawakili wa malengo ya maendeleo endelevu au SDG’s kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Amewaeleza kuwa ajenda ya 2030 na malengo ya maendeleo endelevu ndio mchango mkubwa kwa utandawazi sawia, kwani lengo lake ni kutokomeza umasikini , na ni malengo pekee kuwahi kupitishwa na viongozi wa dunia yanayopigania maslahi ya sayari hii.

Amewahimiza mawakili hao kwamba “tunahitaji hatua , na hatuwezi kuwa na hatua bila uwakili, hivyo jukumu lenu ni muhimu sana.”

Amesisitiza kuzingatia mambo matatu: Mosi uharaka wa utekelezaji wa malengo hayo akisema tayari ni miaka miwili tangu yapitishwe na kuna mda mchache wa kuyatimiza,

Pili ujumuishi wake duniani, kwamba malengo hayo yanamuhusu kila mtu, kila mahali, na hakuna anayeweza kuyatimiza peke yake, na hakuna anayestahili kuachwa nyuma.

Na tatu kutegemeana kwa malengo hayo:, akisema hatua katika lengo moja itasaidia malengo mengine, ikiwa ni pamoja na yanayohusiana na amani na usalama, haki za binadamu na juhudi za masuala ya kibinadamu.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuwajumuisha vijana katika mchakato huu.

Photo Credit
Malengo ya maendeleo endelevu, SDG's. Picha na UM