Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

WHO yafikisha misaada ya kibinadamu Syria

Shirika la Afya Duniani, WHO, limewasilisha zaidi ya tani 11 za vifaa vya matibabu kwa mamlaka za afya katika eneo la Al-Qamishli, kaskazini mwa Syria.

Taarifa ya WHO imesema hii ni mara ya kwanza kwa WHO kusafirisha kwa njia ya anga hadi eneo hilo vifaa vya matibabu tangu mwaka jana.

Vifaa hivyo ni pamoja na dawa za huduma za dharura, dawa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, tembe za dawa za maumivu, virutubisho vya lishe pamoja na viti mwendo.

Makubaliano ya biashara ukanda wa pasifiki, TPP kuleta ahueni- UNCTAD

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema mkataba wa biashara baina ya nchi za ukanda wa Pasifiki, TPP utaleta ahueni kubwa ya biashara na kuwezesha kupunguza bei za bidhaa.

Utafiti wa UNCTAD umebainisha kuwa ingawa ni vigumu kutathmini manufaa ya mkataba huo uliotiwa saini mwezi Februari mwaka huu, bado kunaonekana kuwa angalau bei ya bidhaa itapungua.

Mathalani imesema bei ya nyanya ya chupa inayoagizwa kutoka Chile na kuuzwa kwenye soko la Amerika ya kaskazini itakuwa nafuu kwa asilimia 12 ikilinganishwa na sasa.

Serikali zaahidi kulinda mazingira ya bahari:IMO

Serikali zimetoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi ili kushughulikia taka zinazotupwa baharini hasa za plastiki na chembechembe zingine za plastiki ambazo ni tishio kubwa kwa viumbe na mazingira ya bahari.

Wito huo umetolewa katika mkutano wa 38 wa nchi zilizotia saini mkataba wa London wa ulinzi wa viumbe na mazingira ya bahari. Nchi hizo zimeelezea hofu yake kuhusu suala hilo la taka na plastiki baharini, lakini pia zimesema hatua zimepigwa na baadhi ya nchi katika kuzuia na kushughulikia tatizo la uchafuzi wa mazingira ya bahari utaokanao na taka za plastiki.

India yawa nchi ya 62 kuridhia mkataba wa Paris:

India imekuwa taifa la 62, kuridhia mkataba wa Paris wa mabadiliko yatabia nchi. Akipongeza hatua hiyo ya India kutia saini mkataba Jumapili Oktoba 3 kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa , ambayo pi ni siku ya kimataifa ya kupinga machafuko, Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon amesema

(SAUTI YA BAN)

“Leo serikali ya India imeonyesha mtazamo na uongozi wa kimataifa kwa kujiunga na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi. Hatua hii ya kihistoria inazidi kuimarisha mpango endelevu wa India wa ukuaji na maendeleo”

Utamaduni wa kupinga machafuko, unaanza kwa kuheshimu wengine:Ban

Kila mwaka siku ya kimataifa ya kupinga machafuko hujikita katika kuchagiza amani kwa kufuata mfano wa maisha Mahatma Gandhi ambaye alizaliwa siku hiyo, Oktoba pili , miaka 147 iliyopita. Katika ujumbe maalumu wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon , amesema inafahamika kwamba utamaduni wa kupinga machafuko unaanza na kuwaheshimu wengine, lakini hauishii hapo . Ili kudumisha amani ni lazima kila mtu aheshimu asili.

Chukua msimamo dhidi ya uzee:UM

Umoja wa Mataifa unaadhimisha siku ya kimataifa ya wazee kwa kuzichagiza nchi kutoa kipaumbele na kukabiliana na changamoto ya unyanyapaa na Imani potofu dhidi ya wazee na uzee, na pia kuwawezesha wazee kutambua umuhimu wao katika kuwa na maisha bora ya kiutu na kuzingatia haki za binadamu.

Katika ujumbe wake kwa siku hii ambayo huadhimishwa Oktoba Mosi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema , wakati wazee hufurahia kupewa heshima fulani , ukweli ni kwamba katika jamii nyingi wazee wanatengwa na kutothaminiwa , hali ambhayo inawaathiri pakubwa.

UNHCR na nchi za Afrika wakubaliana hatima ya wakimbizi wa Rwanda,

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na ujumbe kutoka nchi za Afrika , pamoja na Muungano wa Afrika ijumaa wameafikiana hatua za mwisho za kumaliza suala lamuda mrefu la wakimbizi wa Rwanda baada ya miaka saba ya majadiliano.

Mkutano wa mawaziri ulioandaliwa na UNHCR mjini Geneva , umekamilisha hatua ya mwisho ya mchakato wa kina wa mikakati ya suluhu kwa ajili ya wakimbizi wa Rwanda ambao walifungasha virago kati yam waka 1959 na 1998, kukimbia machafuko ya kikabila na vita.