Iwapo ulizikosa wiki hii ya tarehe 18-23 Agosti 2019

24 Agosti 2019

Katibu Mkuu wa UN akaribisha kutiwa saini makubaliano kati ya Uganda na Rwanda. Siku ya kimataifa ya waathirika wa matendo ya vurugu yanayotokana na dini au imani yaadhimishwa kwa mara ya kwanza. "Nitawasamehe lakini nitawauliza, kwa nini mlitaka kunichinja?" asema muathirika wa ugaidi. Tishio la sasa nchini Yemeni ni kubwa zaidi kuliko wakati wowote ule ameonya Martin Griffiths. Ebola yathibitishwa Kivu Kusini, mwanamke mmoja na mwanae wafariki Dunia.

Ebola yathibitishwa Kivu Kusini, mwanamke mmoja na mwanae wafariki Dunia

Mhudumu wa afya anayehusika na kuhudumia wagonjwa wa Ebola akiwa amevalia mavazi sahihi ya kujikinga huku akimlisha mtoto kwenye kituo cha tiba dhidi ya Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC. ( 30 januari 2019)

 

Hatimaye sasa imethibitishwa rasmi kuwa ugonjwa wa Ebola umeingia jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na hivyo kufanya ugonjwa huo sasa kuwa umeenea kwenye majimbo matatu ya taifa hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jumatatu mjini New York, Marekani amesema wagonjwa wamethibitiswa kwenye kijiji cha Chowe Mwenga kusini mwa mji wa Bukavu, jimboni Kivu Kusini.

“Mwanamke mmoja ambaye awali alithibitishwa kuwa na makaribiano na watu wawili waliougua Ebola, wiki iliyopita alisafiri kutoka mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini na kuingia jimboni Kivu Kusini,” amesema Dujarric.

Tishio la sasa nchini Yemeni ni kubwa zaidi kuliko wakati wowote ule- Martin Griffiths

Shaker Ali akiwa amekaa mbele ya lililokuwa eneo la soko mjini Aden, Yemen (Juni, 22, 2019)

 

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, jumanne akihutubia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman,Jordan ameonya kuwa mgawanyiko nchini Yemen umekuwa wenye nguvu zaidi na wa kutisha zaidi kuliko awali.

Mgogoro ulioibuka miaka kadhaa iliyopita kati ya waasi wa Houthi wanaoutawala mji mkuu Sana'a kwa upande wa kaskazini mwa Yemen na pia vikosi vinavyoiunga mkono serikali vikisaidiwa na muungano wa majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia na muungano wa nchi za kiarabu UAE, wameirarua nchi ambayo tayari ilikuwa imeelemewa na matatizo kadhaa ya maendeleo.

Nitawasamehe lakini nitawauliza, kwa nini mlitaka kunichinja?-Muathirika wa ugaidi

Mohammed Lawan Goni, mkimbizi kutoka Nigeria akisali na familia yake katika kambi ya Minawao nchini Cameroon

Mohammed Lawan Goni kutoka Nigeria hivi sasa akiishi katika kambi ya wakimbizi ya Minawao kaskazini mwa Cameroon, anaeleza akisema, “kwasababu ya majanga tuliyoyaona kama vile kuchomwa moto kwa nyumba zetu na mauaji, haifikiriki mtu kurejea Nigeria.”

Mgogoro ulioanzishwa na Boko Haram, umesambaa kutoka jimbo la Borno nchini Nigeria na kuwatawanya takribani watu milioni 10 katika eneo la ukanda wa ziwa Chad.

Siku ya kimataifa ya waathirika wa matendo ya vurugu yanayotokana na dini au imani yaadhimishwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiweka shada la m aua huko Christchurch New Zealand kuenzi waathirika wa shambulio la Machi mwaka huu.

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuadhimisha waathirika wa matendo ya vurugu yanayotokana na dini au imani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ulimwengu unapaswa kupinga na kukataa wale ambao kwa mabavu na kwa uongo wanashawishi kujenga imani potofu, kuchochea mgawanyiko na kueneza hofu na chuki.

Ujumbe wa Bwana Guterres katika siku hii inayoadhimishwa kwa mara ya kwanza leo Agosti 22, umeeleza kuwa, “kwa miezi michache iliyopita, tumeona ongezeko la idadi ya mashambulizi dhidi ya mtu mmojammoja na kulengwa kwa makundi kwasababu tu ya dini au imani zao. Wayahudi wameuawa katika masinagogi, mawe katika makaburi yao yamechorwa alama ya za kibaguzi, waisalamu wamepigwa risasi misikitini, maeneo yao ya kidini yameharibiwa, wakristo wameuawa wakisali, makanisa yao yameteketezwa kwa moto.”

Katibu Mkuu wa UN akaribisha kutiwa saini makubaliano kati ya Uganda na Rwanda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha utiaji saini makubaliano tarehe 21 Agosti 2019 huko Luanda, Angola kati ya marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda kwa minajili ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Amezishauri pande zote kutekeleza makubalano hayo kwa moyo mzuri, kwa lengo la kurejesha urafiki na ushirikiano kati ya majirani hao wawili kwa manufaa ya amani, uthabiti na maendeleo ya kudumu katika kanda hiyo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter