Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matukio ya mwaka 2018 .

Gari ambalo limeharibiwa  na Tsunami katika kijiji cha  Labuhan, Pandeglang, Banten, Indonesia.
UNICEF/Arimacs Wilander
Gari ambalo limeharibiwa na Tsunami katika kijiji cha Labuhan, Pandeglang, Banten, Indonesia.

Matukio ya mwaka 2018 .

Masuala ya UM

Leo Jumatatu ya tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2018, mwisho wa mwaka  jarida la Habari za Umoja wa Mataifa limemulika matukio muhimu ya mwaka huu wa 2018. Hata hivyo tumekuwekea pia habari zilizogongwa vichwa hii leo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Yemen na Afghanistan.

EBOLA

Moja wa matukio yaliyogonga vichwa vya habari barani Afrika ilikuwa ni kuhusu ugonjwa wa Ebola. Mlipuko huo ulitokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DRC.

Mlipuko wa kwanza jimboni Equateur uliripotiwa mwezi Mei na kutokomezwa mwezi Juni, baadaye mwezi  Agosti mlipuko tena jimboni Kivu Kaskazini na hadi leo imeripotiwa kuwa kati ya visa 560, visa 512 vimethibitishwa na kati ya hivyo watu 288 wamefariki dunia kwa Ebola.

Ingawa hivi sasa dawa mpya ya majaribio ambayo ni mkusanyiko wa dawa mbalimbali inatolewa ili kudhibiti ugonjwa huo, kovu la gonjwa hilo kwenye maisha ya watoto waliobakia yatima ni dhahiri .wa watoto yatima ni Stephanie, mtoto mwenye umri wa miaka 10 ambaye mama  yake mzazi amekufa kwa Ebola sambamba na shangazi aliyekuwa anawalea.

SUDAN KUSINI

Mapigano yaliyoanza mwezi Desemba mwaka 2013 na kuleta machungu kwa wananchi sasa yanaonekana kufikia tamati. Hii ni baada ya mashauriano ya miezi 15 ambapo tarehe 12 mwezi Septemba mwaka huu makubaliano mapya ya amani yalifikiwa huko Addis Ababa, Ethiopia kati ya Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar.

Hadi sasa hali  inaelezwa kuwa ni shwari hakuna visa vya mashambulizi kati ya serikali na vikosi vya Machar. Makamanda wa pande zote mbili wakitembelea maeneo ya upande pinzani ambao awali hawakuweza kufanya hivyo. Wakimbizi nao wanarejea nyumbani mathalani huko Akobo mji wa Bor katika jimbo la Jonglei. Mmoja wa wakimbizi hao waliorejea ni Nyaong Nyal Deng ,“baada ya kurejea hapa Akobo, nahisi kama niko nyumbani. Ingawa hakuna chochote, hakuna tatizo. Pengine Mungu atanisaidia, »   amesema.

ROHINGYA

Nako barani barani Asia suala la kurejea nyumbani Myanmar kwa waislamu wa kabila la Rohingya ambao walianza tena kumiminika Bangladesh kusaka hifadhi tangu Agosti 2017 kutokana na mateso na mauaji huko nchini mwao bado halijapata suluhu.

Tangazo la mwezi Novemba kuwa warohingya wanarejeshwa makwao chini ya makubaliano ya utatu kati ya serikali za Bangladesh, Myanmar na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR lilikumbwa na kikwazo.

Iliripotiwa kuwa wakimbizi hao waliandamana tarehe 16 mwezi uliopita wa Novemba huko Cox’s Bazar wakipinga kurejeshwa nchii mwao wakisema kuwa hali ya usalama bado si shwari.

KOFI ANNAN

Mwendazake Kofi Annan, Katibu Mkuu wa 7 wa Umoja wa Mataifa alifariki dunia tarehe 18 Agosti 2018 huko Uswisi na kuzikwa tarehe 13 Septemba Accra, Ghana. Alimwagiwa sifa lukuki na kubwa zaidi Kenya hawatomsahau ambapo kama Balozi Macharia Kamau Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya nje ya Kenya alisema kuwa alikuwa karibu nao wakati wa shida nchini mwao na kuweza kusaidia kutatua na kuleta ufumbuzi kwa vurugu ambazo zilijitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

ULINZI WA AMANI

Na katika masuala ya ulinzi wa amani ambapo wakati wa maadhimisho ya siku ya walinda amani duniani mwaka huu 2018, Umoja wa  Mataifa ulitoa medali ya Dag Hammarskjöld kwa askari 20 wa Tanzania waliouawa wakilinda amani chini ya bendera ya umoja huo. Aliyepokea medali hizo ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero.

Habari nyingine muhimu ni mtanzania aliyeshinda tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2018.  Huyo ni Rebeca Gyumi, akiwa miongoni wa washindi wanne. Tuzo yake alikabidhiwa mwezi Desemba jijini New York .

Halikadhalika mikataba miwili ya aina  yake ilipitishwa mwaka wa 2018 ikilenga kuleta ustawi bora kwa wakimbizi na wahamiaji na kule watokako bila kusahau kule wafikiako.

KATIBU MKUU NA SALAMU ZA MWAKA MPYA

Na bila shaka, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ana tathmini ya mwaka huu wa 2018 kuelekea 2019 akisema..

mwaka mpya uliopita, nilitangaza hali ya tahadhari, na hatari nilizozitaja bado zipo. Hizi ni nyakati za wasiwasi kwa watu wengi, na dunia yetu inapitia katika majaribu mazito. Tunapoanza mwaka huu mpya, hebu na tuazimie kukabiliana na vitisho, kutetea utu wa binadamu na kujenga mustakabali bora—pamoja. Nawatakia nyote na familia zenu mwaka mpya wenye amani na ustawi.”

Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Umoja wa mataifa inatoa shukrani kwako kwa kujumuika nayo mwaka wa 2018 Matarajio ni kuwa utaendelea kuwa nayo mwakani. Pata taarifa zaidi kwenye wavuti news.un.org/sw.  Wafanyakazi wote wa idhaa wanakutakia heri ya mwaka mpya wa 2019

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.