Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO nayo mstari wa mbele kuepusha mizozano kati ya wenyeji na wakimbizi

Rwanda. Mkimbizi mjasiriamali kutoka Burundi ambaye ameweza kujenga upya maisha yake licha ya kuwa mkimbizi.
© UNHCR/Anthony Karumba
Rwanda. Mkimbizi mjasiriamali kutoka Burundi ambaye ameweza kujenga upya maisha yake licha ya kuwa mkimbizi.

FAO nayo mstari wa mbele kuepusha mizozano kati ya wenyeji na wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zikionesha kuwa idadi ya wakimbizi duniani ikiwa ni zaidi ya milioni 70.8, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetaja hatua inazochukua kuepusha mvutano kati ya wakimbizi na wenyeji wao iwe ndani ya nchi zao au ugenini.
 

FAO imesema hatua hizo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa wakimbizi iwe ugenini au ndani ya nchi zao wanakuwa katika mazingira ambayo hawawezi kujipatia kipato na wakati mwingine uwepo wao huibua mazingira ya mvutano na wenyeji.

Julius Jackson ambaye ni mtaalamu wa FAO akihusika na mizozo  isiyoisha ametolea mfano kambi ya Za’atari nchini Jordan ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Syria akisema kwa muwa kambi hiyo imekuwa chanzo cha kiasi kikubwa cha majitaka ambayo yanachafua maji.

Bwana Jackson amesema, “kwa hiyo FAO na wadau wake zikiwemo mamlaka za mitaa, wamekuwa wakibainisha ni kwa vipi tunaweza kugeuza majitaka hayo kuwa kitu cha manufaa au nishati . Hii ikimaanisha kuwa kuna nishati inayozalishwa kwa ajili ya matumizi ya kambini, ambayo kwa sasa haipo. Na hii itaepusha mvutano unaoweza kutokea kati ya jamii hizo na wakati huo huo kufungua fursa za ajira zisizoharibu mazingira kwa wenyeji na wakimbizi .”

Hatua zingine ni miradi ya FAO ya  kuhakikisha kuwa wenyeji na wakimbizi wanapata nishati salama na endelevu badala ya kugombea kuni.

Hata hivyo amegusia pia miradi kama ile ya shirika la mpango wa chakula duniani, WFP ya kuwapatia fedha wakimbizi, fedha ambazo wanatumia maeneo  waliyopo na hivyo kuingiza kipato kwenye jamii akitolea mfano kambi ya Daadab nchini Kenya ambako amesema takwimu zinaonesha kukua kwa pato la ndani kwa asilimia 3 kwenye eneo hilo kutokana na miradi ya usaidizi kwa wakimbizi.

Amepongeza pai nchi za Rwanda na Uganda ambazo amesema zina sera mujarabu zinazoepusha mivutano kati ya wakimbizi na wenyeji ambapo wakimbizi wanahurusiwa kutangamana na jamii na hata kushiriki shughuli za kiuchumi kama wenyeji.