Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tishio la sasa nchini Yemeni ni kubwa zaidi kuliko wakati wowote ule- Martin Griffiths

Shaker Ali akiwa amekaa mbele ya lililokuwa eneo la soko mjini Aden, Yemen (Juni, 22, 2019)
UNHCR/Saleh Bahulais
Shaker Ali akiwa amekaa mbele ya lililokuwa eneo la soko mjini Aden, Yemen (Juni, 22, 2019)

Tishio la sasa nchini Yemeni ni kubwa zaidi kuliko wakati wowote ule- Martin Griffiths

Amani na Usalama

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, hii leo akihutubia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video kutoka Amman,Jordan ameonya kuwa mgawanyiko nchini Yemen umekuwa wenye nguvu zaidi na wa kutisha zaidi kuliko awali.

Mgogoro ulioibuka miaka kadhaa iliyopita kati ya waasi wa Houthi wanaoutawala mji mkuu Sana'a kwa upande wa kaskazini mwa Yemen na pia vikosi vinavyoiunga mkono serikali vikisaidiwa na muungano wa majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia na muungano wa nchi za kiarabu UAE, wameirarua nchi ambayo tayari ilikuwa imeelemewa na matatizo kadhaa ya maendeleo.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Agosti, mapigano yalizuka mjini Aden, ambao ni mji mkuu wa muda wa serikali ya rais Abed Rabbo Mansour Hadi, kati ya makundi mawili yanayopigana dhidi ya waasi wa Houthi. Wapiganaji waliojitenga walitwaa madaraka pamoja na ofisi ya rais kwa siku chache.

Bwana Griffiths, katika hotuba yake kwa wajumbe 15 wa Baraza la usalama amesema, “vurugu zimewaua wananchi wengi na kuwajeruhi mamia. Nina wasiwasi na vurugu hizi na ninalaani juhudi zisizokubalika za Baraza la kusini la mpito, kutwaa taasisi za serikali kwa mabavu. Ninalaani manyanyaso dhidi ya wayemeni wenye asili ya Kaskazini walioko Aden. Kwa upande mwingine ninazikaribisha juhudi za umoja unaoongozwa na Saudi Arabia kurejesha utulivu na kuandaa mazungumzo kati ya pande mbili mjini Jeddah.”

Hakuna muda wa kupoteza

Bwana Griffith amesisitiza kuwa mchakato wa amani ya Yemen ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote na hakuna muda wa kupoteza akisema kuwa, "ninaamini wadau wote wa Yemeni kutoka kanda zote za nchi wataona matukio ya mjini Aden kama daily za wazi kuwa mgogoro wa sasa unatakiwa kukoma haraka na kwa amani.”

 Amani inatakiwa hivi sasa kuliko wakati mwingine: Muller

Naye Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura, OCHA, Ursula Mueller amesema matukio nchini Yemeni yaliyotokea katika wiki chache zilizopita yameonesha kwa mara nyingine namna vita hii ilivyo ya kutisha. Hili liko wazi zaidi katika mateso na kutotendewa haki kwa mamilioni ya raia.

Ametoa mfano akisema “mapema mwezi huu mapigano mjini Aden kati ya serikali na vikosi vya baraza la mpito la kaskazini yaliwaua au kuwajeruhi takribani watu 300 wakiwemo raia wa kawaida. Tunahitajika kwa haraka kuzuia kuendelea kwa mapigano nchini Yemen.”