Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yathibitishwa Kivu Kusini, mwanamke mmoja na mwanae wafariki dunia

Mhudumu wa afya anayehusika na kuhudumia wagonjwa wa Ebola akiwa amevalia mavazi sahihi ya kujikinga huku akimlisha mtoto kwenye kituo cha tiba dhidi ya Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC. ( 30 januari 2019)
WFP/Jacques David
Mhudumu wa afya anayehusika na kuhudumia wagonjwa wa Ebola akiwa amevalia mavazi sahihi ya kujikinga huku akimlisha mtoto kwenye kituo cha tiba dhidi ya Ebola huko Kivu Kaskazini nchini DRC. ( 30 januari 2019)

Ebola yathibitishwa Kivu Kusini, mwanamke mmoja na mwanae wafariki dunia

Afya

Hatimaye sasa imethibitishwa rasmi kuwa ugonjwa wa Ebola umeingia jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na hivyo kufanya ugonjwa huo sasa kuwa umeenea kwenye majimbo matatu ya taifa hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York, Marekani amesema wagonjwa wamethibitiswa kwenye kijiji cha Chowe Mwenga kusini mwa mji wa Bukavu, jimboni Kivu Kusini.

“Mwanamke mmoja ambaye awali alithibitishwa kuwa na makaribiano na watu wawili waliougua Ebola, wiki iliyopita alisafiri kutoka mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini na kuingia jimboni Kivu Kusini,” amesema Dujarric.

Ameongeza kuwa mwanamke huyo na mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitano wamefariki dunia ilhali mtoto wake mwingine mwenye umri wa miezi 7 anapatiwa matibabu.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeripoti ya kwamba kufuatia taarifa hizo lilituma watendaji wake ambao walifiki kwenye kijiji hicho na kutenganisha wanajamii walio na Ebola na kuwapatia matibabu

Halikadhalika walianza kufuatilia waliokuwa na makaribiano na watu hao sambamba na kutoa chanjo na kuwapatia watu elimu kuhusu Ebola.

Ugonjwa wa Ebola bado upo jimboni Kivu Kaskazini na Ituri ambako kasi ya mlipuko ni wastani wa wagonjwa wapya 81 kila wiki.

Hata hivyo msemaji huyo amerejelea kuwa hadi sasa hakuna kisa chochote kilichoripotiwa nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.