Skip to main content

Msighafirike, saidieni DRC ili iondokane na changamoto zake- WHO

Wahudumu wa afya wakipuliziwa dawa kama njia ya kujikinga dhidi ya Ebola baada ya kutoa matibabu huko Beni, DRC. (31  Mei 2019)
Finnish Red Cross/Maria Santto
Wahudumu wa afya wakipuliziwa dawa kama njia ya kujikinga dhidi ya Ebola baada ya kutoa matibabu huko Beni, DRC. (31 Mei 2019)

Msighafirike, saidieni DRC ili iondokane na changamoto zake- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema virusi vya Ebola ni miongoni mwa changamoto lukuki zinazokabili jamii za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kwa hiyo jamii ya kimataifa kuendelea kuonyesha usaidizi na mshikamano na wananchi wa taifa hilo la Maziwa Makuu Afrika.

Msemaji wa WHO, Dkt. Margaret Harris akizungumza na waandishi wa habari mjini  Geneva, Uswisi hii leo, amesema kuwa kado mwa Ebola, bado Surua  nayo ni changamoto akisema kuwa ugonjwa huo tayari umesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000 mwaka huu pekee, idadi kubwa kuliko hata ile ya waliokufa kutokana na Ebola ambayo ililipuka mwezi Agosti mwaka jana.

Tangu Agosti, Ebola imeua watu 1,750 kufuatia mlipuko kwenye jimbo la Ituri na Kivu Kaskazini.

Surua yaonekana kuwa tatizo kubwa kuliko Ebola

“Surua yaonekana kuwa ni tatizo kubwa kuliko Ebola,” amesema Dkt. Harris akisema kuwa hata hivyo “haipo kwenye kipaumbele chao; jamii zinataka barabara nzuri, maji safi, zinapenda kufahamu watoto wao wanaweza kuwa hai hadi umri wa miaka mitano bila kuambukizwa Surua.”

Pamoja na Surua, Malaria na ukosefu wa huduma za msingi, tangu mapema mwezi Juni mwaka huu, zaidi ya watu 300,000  kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini yenye rasilimali lukuki, wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia zinazohusishwa na vikundi vilivyojihami,  imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

Hata hivyo Dkt. Harris ameelezea matumaini yake kuwa hatua ya wiki hii ya kutangaza mlipuko wa Ebola DRC kama jambo la udharura kwa afya ya  umma duniani, unaweza kusaidia kurejesha umakini zaidi katika kusaka mustakabali wa amani na wa kudumu kwa jamii zinazohaha kujikwamua nchini humo.

Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)
UNICEF/Jimmy Adriko
Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)

Msifunge mipaka au kuweka vikwazo vya safari DRC

Msemaji huyo akiangazia dunia amesema pendekezo kuu ni “kusaidia DRC na si  kuchanganyikiwa. Msifunge mipaka. Msiweke vikwazo vya safari au vya biashara. msichanganyikiwe.”

Akitambua kuwa jopo la wataalamu wa WHO lililotangaza tahadhari hiyo lilitambua uwezekano wake wa kuathiri uchumi wa DRC,Dkt. Harris amesema, “hadi sasa ulimwengu umekuwa mwema kwa kutoitengea nchi hiyo ya Afrika ya Kati.”

Mchuuzi wa samaki aliyeambukizwa Ebola hakusafiri kwenda Rwanda

Mapema, afisa wa WHO alithibitisha kuwa mchuuzi wa samaki kutoka DRC aliyekuwa ameambukizwa Ebola na hatimaye kufariki dunia, hakusafiri kwenda Rwanda mapema mwezi huu licha ya taarifa za awali za mkanganyiko kuhusu suala hilo. 

Dkt. Harris amesema kuwa mchuuzi huyo alisafiri kutoka Beni nchini DRC na kuelekea sokoni Uganda kama afanyavyo siku zote lakini alikuwa anaugua kupindukia na alirejeshwa kwao na kufariki dunia siku nne baadaye.

“Taarifa potofu ya kwamba alizuru Rwanda zilitoka mamlaka ya Uganda kabla ya kuchapishwa katika wavuti wa WHO,” amesema Dkt. Harris .

Kila mwezi, takribani watu 1,100 huvuka mpaka kutoka DRC na kuingia Rwanda ambapo kwa mujibu wa WHO, bado wako makini ya kwamba timu zake za ufuatiliaji zina uhakika kuwa virusi vya Ebola havikuingia Rwanda.