Nitawasamehe lakini nitawauliza, kwa nini mlitaka kunichinja?-Muathirika wa ugaidi

21 Agosti 2019

Leo ni siku ya kimataifa ya kumbukizi na kutambua waathirika na manusura wa vitendo vya ugaidi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza kwenye makao makuu ya chombo hicho jijini New York, Marekani amesema ugaidi na aina zake zote umesalia changamoto kubwa.

Amesema ugaidi umebakisha makovu ya kudumu kwa manusura na familia zao akiongeza kuwa ingawa muda unakwenda bado makovu hayo katu hayaishi ambapo miongoni mwa mashuhuda wa kauli hiyo ya Bwana Guterres ni Mohammed Lawan Goni ambaye anasema hayuko tayari kurejea nchini mwake Nigeria ingawa yuko tayari kuwasamehe waliomtendea maovu. 

Mohammed Lawan Goni kutoka Nigeria hivi sasa akiishi katika kambi ya wakimbizi ya Minawao kaskazini mwa Cameroon, anaeleza akisema, “kwasababu ya  majanga tuliyoyaona kama vile kuchomwa moto kwa nyumba zetu na mauaji, haifikiriki mtu kurejea Nigeria.”

Mgogoro ulioanzishwa na Boko Haram, umesambaa kutoka jimbo la Borno nchini Nigeria na kuwatawanya takribani watu milioni 10 katika eneo la ukanda wa ziwa Chad.

Mohammed anaeleza kuwa alikamatwa na Boko Haram, akateswa sana. Nyumba yake ilichomwa moto. Na sasa hataki kurejea Nigeria hadi Boko Haramu watakapodhibitiwa.

Alikuwa mkusanya kodi kabla hajakamatwa. Anaeleza, “waliingia katika mji wetu saa kumi alfajiri wakaanza kuwarushia watu risasi na kuchoma nyumba. Wanishika na kunipeleka kichakani, wakanifunga mikono wakitaka kunichinja wakisema ninaifanyia kazi serikali lakini Allah aliniokoa. Wanaume fulani walionifahamu walikuja wakawasihi walioniteka waniachie. Waliniachia, nikakimbia nikaanguka katika mto nikavunjika mguu.”

Mohammed atimaye aliweza kuvuka na kuingia Cameroon. Anasema wawili kati ya waliotaka kumchinja walikuwa wanatoka katika mji wake, na wawili kutoka Maiduguri.  Anasema nikiwaona nitawasamehe lakini nitawauliza, kwa nini mliwachinja watu mbele yangu? Kwa nini mlikuja na kisu mkitaka kunichinja?

Zaidi ya wakimbizi wa Nigeria takribani 57,000 wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Minawao huko Cameroon. Na kambi hiyo inaendelea kuwapokea idadi kubwa ya wakimbizi wanaowasili.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter