Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

La Nina yaweza kugonga pembe ya Afrika

Ukame unaotokana na El Niño umeathiri sana Arsi, Ethiopia mwaka 2016. Picha: OCHA / Charlotte (maktaba)

La Nina yaweza kugonga pembe ya Afrika

Mwaka 2018 unapoanza huku majanga ya asili yakiwa hayakwekepi, ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa majanga, OCHA imetaka hatua zaidi ili kuepusha madhara yatokanayo na El Nino na La nina.

Afisa mwandamizi wa OCHA Greg Puley amesema hayo akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akigusia zaidi El niño ambayo husababisha kubadilika kwa joto la bahari na kuleta mtafaruku katika maeneo mengi duniani ikiwemo joto kali ambalo husababisha mvua kubwa pamoja na La nina ambayo huleta mkondo wa baridi baharini.

Ametolea mfano matukio mawili makubwa ya El Niño miaka miwili iliyopita ambapo ilisababisha madhara kwenye nchi 23 huku watu milioni 60 wakisaka msaada wa dharura.

Bwana Puley amezungumzia pia madhara ya La nina ambayo kuna uwezekano wa asilimia 70 ikaleta madhara makubwa hasa kwenye ukanda wa pembe ya Afrika ikiwemo Somalia na maeneo ya Kenya.

(Sauti ya Greg Puley)

“Maji yanapungua, hakuna malisho ikimaanisha rasilimali zao za kaya zinapungua zaidi. Watu hawa wataaamua kuchukua hatua hasi ikiwemo kuuza mifugo au rasilimali zao. Hawa ni watu ambao watahitaji msaada zaidi.” 

Hivyo amesema OCHA jukumu lake ni kushirikiana na serikali kuweka mifumo bora ya utabiri wa kile kinachoweza kutokea kwa kuwa ..

(Sauti ya Greg Puley) 

“Kadri tunavyoweza kuchukua hatua mapema ndivyo hatua hiyo itakuwa fanisi na yenye tija. Hatutaki ifike kwenye hali mbaya ya kibinadamu ambapo tunaanza kugawa vyakula zaidi au maji. Iwapo tutachukua hatua mapema tutapunguza hali kuwa mbaya zaidi.”