Somalia yapokea vifaa vya tiba ya dharura baada ya shambulio la Jumamiosi: WHO

17 Oktoba 2017

Shirika la afya ulimwenguni WHO limewasilisha vifaa vya tiba na huduma ya dharura ikiwemo damu ya kuokoa maisha baada ya shambulio la bomu Jumamosi Oktoba 14 mjini Moghadishu.

Takribani watu 300 wameuawa na mamia kujeruhiwa katika shambulio hilo. Vifaa vingine vilivyowasili ni pamoja na vikasha vya kupimia kundi la damu, vifaa vya kuwahudumia waliokumbwa na kiwewe, madawa, vufaa vya huduma ya kwanza na vifaa vinginevyo , viliwasilishwa haraka kwenye hospitali ambako madaktari na wauguzi walijikuta katika taharuki baada ya idadi ya maiti na majeruhi waliokuwa katika hali mahtuti kuongezeka kwa kasi.

Vifaa hivyo vilivyowasili kwa ujumla vitaweza kutumika kufanya vipimo 500 vya damu na kuwapa tiba ya haraka wagonjwa 100 waliokumbwa na kiwewe na wanaohitaji huduma ya dharura.