Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata wapunguza chakula kwa wakimbizi wa Burundi na DRC: Rwanda

Perus na watoto wake katika kambi ya Mugombwa kusini mwa Rwanda. Ni wakimbizi kutoka DRC. Picha: UNHCR

Ukata wapunguza chakula kwa wakimbizi wa Burundi na DRC: Rwanda

Mashirika ya Umoja wa Mataifa-la mpango wa chakula duniani(WFP) na la kuwahudumia wakimbizi (UNHCR) yameomba msaada zaidi kutoka kwa wahisani ili kukabili upungufu wa mgao wa chakula uliopo kwa wakimbizi walioko nchini Rwanda.

Wito huo umechochewa na ukata wa pesa za kutosha kuweza kutoa msaada kamili wa chakula unaohitajika na wakimbizi takriban 130 elfu kutoka Burundi na Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo DRC, walioko nchini Rwanda.

Mgao wa chakula  pamoja na msaada wa kifedha wa asilimia 25, ulipunguzwa , ilihali wakimbizi baado wapo. Wakimbizi kutoka DRC na Burundi waishio katika kambi nchini Rwanda hutegemea mno msaada kuweza kukidhi mahitaji yao ya chakula.

Kawaida wakimbizi hao hupokea aidha chakula au pesa, kila mwezi ,kutoka kwa WFP ili kuweza kununulia chakula katika masoko ya karibu.

Mkuu wa ofisi ya WFP nchini Rwanda, Jean- Pierre de Margerie, amesema kuwa mbali na kuwashukuru  wahisani kwa ukarimu wao, hata hivyo anawaomba kuendelea na  kufadhili misaada  zaidi ya kibinadamu ili shirika lake liweze kutoa msaada unaotarajiwa kwa wakimbizi hao.

Kabla ya Novemba mwaka 2017 WFP lilikuwa  inatoa kilo karibu 17 za chakula kwa kila mkimbizi kwa mwezi, ilhali wakimbizi wengine wakipokea faranga za Rwanda 7,600, ambazo ni sawa na dola 9 za kimarekani kuweza kununua chakula katika masoko ya kawaida.Na sasa shirika hilo limelazamika  kupunguza msaada hadi asilimia 90 kwa mwezi Novemba na Disemba.