Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ndani ya Syria ina taswira tofauti-De Mistura

Hali ndani ya Syria ina taswira tofauti-De Mistura

Staffan de Mistura, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria ametoa taarifa hii leo kwenye baraza la usalama kuhusu mchakato wa amani katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Amesema hali ndani ya Syria ina taswira tofauti, na wakati kukiwa na maendeleo chanya kwa kiasi fulani, pia taifa hilo liko katika majaribio ya endapo utashi wa kisiasa kwani utashikilia nia ya kupunguza machafuko na kuwa na mjadiliano yenye maana.

De Mistura amesema kwa hakika wimbi la machafuko limepungua tangu kutiwa saini makubaliano ya kupunguza machafuko mwezi Mei, hata hivyo amesema katika baadhi ya maeneo mapigano yanaendelea na hata kushika kasi, pia kuimarisha kwa usalama hakujanufaisha fursa za misaada ya kibinadamu.

(SAUTI YA DEMISTURA)

“Kila wiki inayopita tunafahamu bila kuhitimishwa muafaka wa mwisho wa maeneo ya kupunguza machafuko, hali tete na tishio la usitishaji uhasama linaongezeka.”

De Mistura amezungumzia pia duru nyingine ya mazungumzo itakayofanyika mwezi ujao mjini Geneva Uswis na kupendekeza kufanya mazungumzo mengine August au mapema Septemba kabla ya kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa na kwamba atahudhuria mazungumzo yatakayofanyika Astana Julai 4-5.

(SAUTI YA DEMISTURA)

“Natumai kwamba mchanganyiko wa mambo haya utasaidia kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo ya Syria mjini Geneva, katika miezi ijayo na kutufikisha hatua moja mbele katika safari ya lengo la pamoja la utekelezaji wa maazimio ya baraza hili na hususani nambari 2254.”

Azimio la baraza la usalama nambari 2254 lilipitishwa mwaka 2015 na limeweka mkakati wa mchakato wa amani ya Syria unayojumuisha majadiliano na usitishaji uhasama nchi nzima.