Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ECOSOC yapata Rais mpya, azungumzia malengo ya maendeleo ya milenia

ECOSOC yapata Rais mpya, azungumzia malengo ya maendeleo ya milenia

Baraza la kijamii na kiuchumi la Umoja wa Mataifa, ECOSOC leo limepata Rais mpya Martin Sajdik, ambaye ni mwakilishi wa kudumu waAustriakwenye Umoja wa Mataifa. Anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Balozi Néstor Osorio, mwakilishi wa kudumu waColombiakwenye Umoja wa Mataifa ambaye amemaliza muda wake.

Mara baada ya kuchaguliwa, Balozi Sajdik alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuangazia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia hasa kusaidiana na nchi zinazoendelea ambazo zinajitahidi kufikia malengo hayo.

Amesema zikiwa zimebakia chini ya siku 700 kufikia ukomo wake, kuelekeza nguvu kwenye malengo hayo ni muhimu kwani kunatoa mazingira bora ya kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.

(Sauti ya Balozi Sajdik)

“Nafikiri ni muhimu kuonyesha kuwa kadri nchi zinavyojitahidi kufikia malengo ya milenia, ndivyo ambavyo inakuwa rahisi kufikia pia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Kwa hivyo basi ni muhimu kuongeza kasi kwenye kipindi hiki cha siku 700 au chini ya hapo na kujitahidi kwani unapotimiza vyema malengo ya milenia ndivyo itakuwa rahisi kipindi cha mpito cha SDGs.”

Balozi Sajdik anachukua akiwakilisha ukanda wa Ulaya Magharibi na nchi nyinginezo atashika wadhifa huo hadi mwezi Julai mwaka 2015.