Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa-OCHA

Mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa-OCHA

Shambulio dhidi ya msafara wa misaada Syria lililosababisha dereva mmoja kujeruhiwa limelaaniwa vikali na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA na kusema ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa Jens Laerke msemaji wa shirika hilo, majeruhi ambaye ni mfanyakazi wa shirika la hilali nyekundu nchini Syria alikuwa akijaribu kupeleka msaada Harasta Mashariki karibu na Damascus mwishoni mwa juma alipopigwa risasi baada ya kulazimishwa kugeuka nyuma na sasa ingawa yuko mahtuti lakini yu salama baada ya kufanyiwa upasuaji.

Dereva wa pili pia alijeruhiwa pia katika msafara huo ambao hatimaye ulifanikiwa kuwasili Harasta Mashariki ukiwa ni wa kwanza tangu 29 Oktoba 2016.