Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwe makini udhibiti wa ugaidi usichochee machungu- Guterrres

Tuwe makini udhibiti wa ugaidi usichochee machungu- Guterrres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kadri vitisho vitokanavyo na misimamo mikali vinavyozidi kuchanua, ni vyema kuhakikisha mbinu za kudhibiti hazileti matatizo.

Bwana Guterres amesema hayo leo huko Ashgabat, Turkmenistan kwenye kikao cha ngazi ya juu cha kutathmini jinsi mataifa ya Asia ya Kati yanavyotekeleza mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na ugaidi.

Amesema ni vyema kudhibiti lakini jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa mipango yote ya kukabili ugaidi inazingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Kwa mantiki hiyo amesema juhudi za kudhibiti zijumuishe makundi yote ya jamii hususan yale yanayokabiliwa na machungu ya ubaguzi na kuwekwa pembezoni.

Katibu Mkuu amepongeza jinsi mataifa matano ya eneo hilo yaliyoridhia azimio la Ashgabat mwaka 2011 la kutekeleza mkakati huo wa Umoja wa Mataifa akisema hatua hiyo imekuwa mfano kwa mataifa mengine duniani.