Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Faida za wahamiaji za kiuchumi zitambulike: UM

Faida za wahamiaji za kiuchumi zitambulike: UM

Likizingatia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi na wahamiaji wa hivi karibuni, baraza la haki za binadamu hii leo mjini Gweneva Uswisi, limekuwa na mjadala shirikishi kuhusu haki za kundi hilo katika muktadha wa kuhama kwa makundi makubwa.

Wajumbe wa baraza hilo wamesisitiza kuwa kuheshimu haki za binadamu kwa wahamiaji sio tu hitaji la kisheria bali pia ni jambo lenye busara kulitekeleza, wakitolea mfano wa kuwaengua wahamiaji katika mfumo wa afya, elimu na siasa au kuwaeka kizuizini huongeza gharama katika safari yao na nchi watakazofikia.

William Lacy Swing, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataiafa la uhamiaji IOM, ameliambia baraza hilo kuwa kuna mtizamo hasi wa kutotambua mchango wa kiuchumi unaotekelezwa na wahamiaji katika jamii kadhaa, na kutaka jumuiya ya kimataifa kupigia chepuo sera ya watu kuhama kihalali.

Mmoja wa wajumbe amesema ni muhimu kuzipinga sera nyanyapazi dhidi ya wahamiaji, na kuanza kuzungumzia zaidi faida za uhamiaji katika nchi zinazowapokea.