Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasaidia raia zaidi ya milioni moja kaskazini mashariki mwa Nigeria

WFP yasaidia raia zaidi ya milioni moja kaskazini mashariki mwa Nigeria

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema kuwa tangu mwanzo wa mwezi huu wa Desemba, limetoa msaada wa chakula au fedha kwa zaidi ya raia milioni moja katika maeneo yenye vita kwa walioathirika katika Kaskazini mashariki mwa Nigeria.  Hii inamaanisha kwamba zaidi ya nusu ya wale wanaohitaji msaada wa kibinadamu kwa haraka sasa wamefikiwa.

Hatua hii inakuja wakati shirika hilo linawasaidia raia katika majimbo ya Borno na Yobe nchini Nigeria ambako takriban watu milioni nne wana uhaba wa chakula.

Maeneo haya yamekuwa na vurugu kwa miaka mingi na kukumbwa na mashambulizi ya  kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ambapo zaidi ya nusu ya watoto wote chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo.

Mwakilishi wa shirika hilo nchini Nigeria na mratibu wa misaada ya dharura Sory Ouane ameshukuru serikali na wadau wote wa misaada ya kibinadamu akisema kuwa hii imewapa fursa kuongeza idadi ya watu waliopata msaada.

Katika maeneo yenye masoko, zaidi ya watu 170,000 walisaidiwa na fedha taslimu.

Takriban watu 800,000 - wengi wao waliokimbia makazi yao katika kambi au kwa jamii wamenufaika kutokana na mgao wa chakula; na karibu watoto 180,000 chini ya miaka mitano walipewa chakula bora maalum.

WFP inahitaji dola milioni 208 kuweza kutoa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Nigeria katika kipindi cha miezi sita na kati ya hizo bado dola million 143 bado hazijapatikana.