Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangura awataka wanaozozana Sudan Kusini wazuie ukatili wa kijinsia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika vita, Zainab Hawa Bangura(Picha ya UM/maktaba)

Bangura awataka wanaozozana Sudan Kusini wazuie ukatili wa kijinsia

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kijinsia katika maeneo ya migogoro, Bi Zainab Hawa Bangura, amehitimisha ziara yake ya kwanza Sudan Kusini kwa taarifa ya pamoja na serikali ya kuonyesha hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kuzuia na kushughulikia uhalifu wa kijinsia, akisema, pande zote katika migogoro zinahusika katika kitendo hicho.

Katika taarifa hiyo, Bangura amesema alichoshuhudia katika eneo la Bentiu ndicho kitu kibaya zaidi yeye kuwahi kuona katika kipindi cha miaka 30 ya kukabiliana na suala hili, akisema hii ni kwa sababu ya mchanganyiko wa ukosefu wa usalama wa muda mrefu, hali mbaya ya kupindukia ya maisha, wasiwasi wa ulinzi wa kila siku na unyanyasaji wa kijinsia uliokithiri.

Akimnukuu mwanaharakati mwanamke aliyekutana naye, Bi Bangura ameongeza kuwa miili ya wanawake na watoto imegeuzwa kuwa ni uwanja wa vita katika mgogoro huo, akielezea kuwa sio ubakaji pekee, bali kuwapa machungu na uharibifu

Bagura alikutana na Rais Salva Kiir, wakati wa mwanzo na mwisho wa ziara yake, na alaifanya mashauriano ya kina na mawaziri husika ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi.

Aidha, alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Sudan Kusini, vikundi vya wanawake, viongozi wa jamii, wahudumu wa kibinadamu, waandishi wa habari na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.