Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni Moja zahitajika kukwamua wahitaji Nigeria

Dola bilioni Moja zahitajika kukwamua wahitaji Nigeria

Ombi la zaidi ya dola Bilioni Moja limetangazwa ili kusaidia jamii nchini Nigeria zilizoachwa bila kitu kufuatia vitendo vya Boko Haram.

Naibu mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Nigeria Peter Lundberg ametaja majimbo yenye uhitaji zaidi kuwa ni Borno, Yobe na Adamawa.

Amesema kinachoendelea ni janga la ulinzi linalotokana na athari za mzozo, janga ambalo amesema sasa linageuka kuwa janga la lishe na uhakika wa chakula.

Bwana Lundberg amesema kwa sasa kuna fursa ya kushughulikia janga hilo kwa kukidhi mahitaji husika na kwa kufanya hivyo kutaepukwa gharama za ziada.

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu Milioni Nane na nusu kaskazini-mashariki mwa Nigeria wanahitaji msaada wa chakula, malazi na huduma nyingine muhimu.

Mahitaji yao yanaendelea kubainika siku hadi siku kadri jeshi la Nigeria linavyokomboa maeneo ambayo awali yalikuwa yanashikiliwa na Boko Haram.