Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nusu ya watu wa Juba hawana uhakika wa chakula: OCHA

Zaidi ya nusu ya watu wa Juba hawana uhakika wa chakula: OCHA

Utafiri mpya uliofanywa na washirika wa masuala ya chakula na lishe unaonyesha kwamba watu takribani 260,000 mjini Juba Sudan Kusini ama wana chakula kidogo sana au hawana uhakila na mlo wao.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA inasema hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula mjini Juba imeongezeka mara mbili tangu Julai mwaka jana.

Imeongeza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya kaya zimegeukia msaada wa dharula kama njia ya kuishi ikiwa ni pamoja na kukopa chakula, kula mlo mmoja kwa siku na wakati mwingine kutokula kabisa au kula vyakula vya porini.

OCHA inasema lawama za hali hii zinaelekwezwa kwa mfumuko wa bei, kushuka kwa pauni ya Sudan Kusini, upotevu wa fursa za ajira na kupungua kwa uwezo wa watu kununua bidhaa.