Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za uwekezaji zizingatie udhibiti wa uchafuzi wa hewa- Ban

Sera za uwekezaji zizingatie udhibiti wa uchafuzi wa hewa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema uchangishaji fedha na uwekezaji ndio ufunguo wa kufanikisha kupunguza kwa gesi chafuzi, ulimwenguni.

Amesema hayo huko Marrakesh, Morocco katika hotuba iliyowasilishwa na mshauri wake wa masuala ya tabianchi, Robert C. Orr mbele ya washiriki wa kikao cha ngazi ya mawaziri wa mkutano wa 22 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP22.

Kikao kimeangazia uchangishaji fedha kwa miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi ambapo Ban hata hivyo amesema uwekezaji huo uzingatie miradi isiyochafua mazingira, akitaja miradi ya miundombinu itakayogharimu dola trilioni 90 katika miaka 15 ijayo.

Amesema iwapo uwekezaji utaenda sambamba na sera bora za kufanikisha kiwango kidogo cha hewa chafuzi na dunia inayoweza kukabilia mabadiliko ya tabianchi, hiyo itafungua mipango ya ulimwengu salama na wenye afya na endelevu kwa vizazi vijavyo.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa kwenye mkutano na viongozi wa Afrika. (Picha:COP22)
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alizungumza kwenye kikao cha viongozi wa Afrika kilichoandaliwa na mfalme Mohammed wa VI wa Morocco ambapo amesema ametaka nchi ambazo haziridhia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi zifanye hivyo hima.

Amesema ameshuhudia miradi bunifu barani Afrika ya kukabili mabadiliko ya tabianchi akisema sasa kilichosalia ni vijana ambao wako mstari wa mbele wawezeshwe ili wafanikishe utekelezaji wa mkataba huo.

(Sauti ya Ban)

"Kuna vijana wanaoleta matumaini makubwa kwenye nchi zenu. wanahitaji uwekezaji na wana haki ya kuwezeshwa. wakipatiwa fursa sahihi, vijana wa Afrika wanaweza kuibuka na suluhu ambazo hatuwezi hata kufikiria."