Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Enzi mpya ya utekelezaji na hatua" kuhusu mabadiliko ya tabia nchi:COP22

"Enzi mpya ya utekelezaji na hatua" kuhusu mabadiliko ya tabia nchi:COP22

Nchi zilizokusanyika kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia au COP22 , zimetangaza tamko la “enzi mpya ya utekelezaji na hatua kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.”Tamko la hatua la Marrakech, limetolewa leo Ijumaa siku ya mwisho ya mkutano huo uliokunja jamvi nchini Morocco, likisema, jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa haraka wa kuchukua hatua dhidi ya dunia inayozidi kuchemka , ili kuhakikisha kiwango cha joto kinasalia chini ya nyuzi joto 2 celsius.

Tamko hilo lililoafikiwa na wakuu wan chi, serikali na wajumbe wote waliokusanyika linasema kuna kasi nzuri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kote duniani , kasi ambayo haibadiliki, likiongeza kwamba inachagizwa sio tu na serikali bali na sayansi, biashara, na hatua za kimataifa za aina zote na katika viwango vyote.

Tamko hilo linatoa wito kwa wadau wote kujenga kasi ya kwenda sanjari na mabadiliko lengo la kufikia utekelezaji wa ajenda yam waka 2030. Waziri wa mambo ya nje wa Morocco Salaheddine Mezouar ndiye aliyekuwa Rais wa mkutano huo wa COP22 akizungumza kwenye mkutano wa mwisho na waandishi wa habari amesema mkutano huo

(SAUTI YA MEZOUAR)

"Ilikuwa hali halisi, lakini pia azimio la dhamira ya jumuiya ya kimataifa kwa vita hii dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Pia ni uthibitisho kwamba kipaumbele kitolewe kwa hatua na kwa utekelezaji. Maslahi lazima yaelekezwe kwa walio katika nchi zilizo kwenye mazingira magumu zaidi na nchi zinazoendelea. "

Katika siku hii ya mwisho ya mkutano kundi la nchi zaidi ya 45 zimekuja pamoja kama kongamano la walio katika wakati mgumu na mabadiliko ya hali ya hewa na kutangaza ajenda yao ya kutekeleza mkataba wa Paris na wakiwa na lengo la kuhakikisha wakuwa na kiwango cha joto cha nyuzi joto 1.5, iliyokuwa kabla ya mapinduzi ya viwanda.