Hali ya hewa iliyokithiri inachangiwa na ongezeko la joto duniani: WMO
Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO , limechapisha ripoti ya uchambuzi wa kina wa hali ya hewa kimataifa kwa mwaka 2011 -2015 , ikiwa ni miaka mitano iliyokuwa na joto kali katika historia. Shirika hilo linasema kumekuwa na ongezeko dhahiri la mchango wa binadamu katika hali ya hewa iliyokithiri na matukio mbalimbali yenye hatari kubwa na gharama kwa dunia nzima.
Kumekuwa na viwango vya juu vya joto vilivyoambatana na kupanda kwa kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu Arctic, na theluji kwenye ncha ya kazikazini mwa dunia. WMO inasema mabadiliko yote haya ya tabia nchi yanathibitisha ongezeko la joto la muda mrefu linalosababishwa na gesi chafuzi, huku kiasi cha hewa ya ukaa (CO2) kikifurutu ada mwaka 2015.
Ripoti hiyo “Hali ya hewa ya kimataifa 2011-2015” pia inatathimini endapo kuna uhusiano baina ya mabadiliko ya tabia nchi yasababishwayo na binadamu na matukio ya hali ya hewa yaliyokithiri, na tafiti 79 zimefanyika. Zaidi ya nusu ya tafiti hizo zimebaini kwamba mabadiliko yatokanayo na mchango wa binadamu yanasababisha hali ya hewa iliyokithiri ikiwemo joto la kupindukia.
Ripoti imetaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni ukame Afrika Mashariki 2010-2012, mafuriko Kusini mwa asia 2011, joto la kupindukia India na Pakistan 2015, kimbunga Sandy 2012 na kimbunga Haiyan kilichoikumba Ufilipino mwaka 2013
Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi ulioanza kutekelezwa tarehe 4 Novemba umekamia kupungua kiwango cha jot o duniani na kufikia chini ya nyuzi joto 2 °C.