Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapotofu wenye misimamo mikali ni lazima wakabiliwe:Zeid

Wapotofu wenye misimamo mikali ni lazima wakabiliwe:Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein amesema ni aibu kwamba, wahanga wa mateso yenye kuchukiza, walazimike tena kuteseka zaidi kutokana na ukosefu wa ulinzi wa jamii ya kimataifa.

Bwana Zeidi amesema hayo katika hotuba yake wakati wa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu wimbi la wakimbizi na wahamiaji uliofanyika leo jijini New York, Marekani.

Amesifu kazi nzuri ya maandalizi ya mkutano huu iliyofanywa na Katibu Mkuu Ban na wadau wengine, lakini amekumbusha kwamba mkutano huu usiishie tu kuwa hotuba, mapambo na pongezi za kibinafsi.

Ameongeza kuwa, hakuna faraja ikiwa matumaini ya uhuru wa mamilioni ya watu ni mahema, kubeba watoto na mizigo yao mgongoni, kutembea maili mia au elfu, kuzama, na wakifika, kutupwa rumande kwenye hali mbaya na wanapoachiliwa kukumbwa na chuki na ubaguzi.

(Sauti ya Zeid)

"Ukweli mchungu ni kwamba , mkutano huu uliitishwa kwa sababu tumeshindwa kwa kiasi kikubwa. Tumeshindwa kuwasaidia wanaoteseka kwa muda mrefu Syria, kutokana na kutokumaliza vita wakati wa uchanga wake. Kushindwa kuwasaidia wengine walio katika migogoro sugu, kwa sababu hiyo. Kushindwa kusaidi mamilioni ya wahamiaji ambao wanastahili maisha zaidi ya, kuvunjiwa heshima na kukata tamaa kuanzia utotoni hadi kaburini".

Kwa mantiki hiyo, amesema mabadiliko yanawezekana, lakini hayataweza kufikiwa iwapo wale wenye kupigania haki zao wamezungukwa na wale wenye kuhubiri siasa za chuki na uongo kwa maslahi yao na wafuasi wao, akiwasisitizia kuwa ..

(Sauti ya Zeid)

"Kama mko hapa , tunawaeleza tutaendelea kuwtaja majina yenu hadharani. Mnaweza kuondoka kwenye ukumbi huu, lakini hamuwezi kukimbia hukumu ya walio wengi kwenye dunia hii.”