UNHCR yatiwa wasiwasi na hali Aleppo na mashambulizi Idleb

UNHCR yatiwa wasiwasi na hali Aleppo na mashambulizi Idleb

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limetoa wito kwa pande kinzani nchini Syria kuhakikisha usalama na hadhi ya raia, na watu wote walionaswa katika mji wa Aleppo, ambao wanakabiliwa na mashambulizi ya bomu, ukatili na kulazimika kuhama.

Aidha, UNHCR imeeleza kutiwa wasiwasi na visa vya mashambulizi dhidi ya makazi ya wakimbizi wa ndani katika mkoa wa Idleb nchini humo katika kipindi cha siku 10 zilizopita, pamoja na mashambulizi dhidi ya maeneo mengine nchini wanakokaa wakimbizi na raia, ambayo yamesababisha vifo na majeraha.

Shirika hilo limesema mashambulizi hayo yanaonyesha kutothamini maisha ya raia, likikariri umuhimu wa kuhakikisha raia wanaruhusiwa kuweza kuyafikia maeneo salama, na kuheshimu hulka ya kiraia na kibinadamu ya makazi ya wakimbizi wa ndani.

Aidha, UNHCR imekariri wito wake wa kuhakikisha kuwa raia wanalindwa kwa misingi ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, sheria ya wakimbizi, na sheria ya haki za binadamu.