Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati si muafaka kwa mazungumzo kuhusu Syria- de Mistura

Wakati si muafaka kwa mazungumzo kuhusu Syria- de Mistura

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura amesema wakati sasa si muafaka kurejea mazungumzo juu ya mustakhbali wa nchi hiyo licha ya dalili za maendeleo katika mchakato wa kupeleka misaada.

De Mistura amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi akitaja sababu kuwa ni kutokuwepo kwa maendeleo ya kutosha kwenye suala la msingi la mpito wa kisiasa.

Amesema aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa nia yake ni kuona mazungumzo yanarejea lakini ni lazima yaweze kuwa na matokeo thabiti.

Tuantaka kuweka fursa ya kuwa na matokeo thabiti. Na matokeo thabiti ni yapi? Kuanza kabisa kwa kipindi cha mpito wa kisiasa kivitendo na si kwa maneno.Na hii ina maana kwamba tunahitaji aina ya jambo la msingi linaloandaliwa kwa majadiliano siyo na sisi peke yetu, bali na nchi kubwa. Na kwa mtazamo wangu mazingira hayo bado hayajawadia.”

Bwana de Mistura amesema licha ya kutokuwepo kwa mazungumzo ya Geneva, mijadala ya kiufundi na mtu yeyote mwenye nia ya kuchangia amani kwa Syria itaendelea.

Ameongeza kuwa tarehe Mosi Agosti ambayo ilipendekezwa na kikundi cha kimataifa cha usaidizi wa Syria iwe siku ambayo kipindi cha mpito wa kisiasa kiwe kimeanza Syria, bado ni jambo linaloweza kufikiwa.