Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ana haki ya kujitambulisha apendavyo kazini- ILO

Kila mtu ana haki ya kujitambulisha apendavyo kazini- ILO

Leo ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Chuki dhidi ya Wapenzi wa Jinsia moja na wanaojitambulisha kwa jinsia tofauti na maumbile yao (LGBT), Shirika la Kazi Duniani (ILO), limetilia mkazo umuhimu wa haki ya kijamii na ajira za kiutu kama viungo muhimu vya afya na maisha bora, na kielelezo cha haki za watu hao. Taarifa kamili na Flora Nducha

(Taarifa ya Flora)

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni afya ya akili na maisha bora.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder, kauli mbiu hiyo inafaa hasa kwa sababu miaka 26 iliyopita siku hii, Shirika la Afya Duniani (WHO), lilitengua kuorodheshwa kwa mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa matatizo ya akili.

Amesema utaifiti uliofanywa na ILO na mashirika mengine, umebainisha kuwa wafanyakazi wengi wa LGBT huficha mwelekeo wao kimapenzi, na hilo huchangia msongo wa akili, huzuni, na kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS), Michel Sidibe, ametoa wito watu wa LGBT wawezeshwe kikamilifu kupata huduma bora za afya, zikiwemo za afya ya akili.

(SAUTI YA SIDIBE)

“Wanatengwa, wanakabiliwa na ukatili, wanaishi kwa uoga, na kwa kujificha. Hawawezi kupata huduma za afya za kuokoa maisha. Haikubaliki kwamba watu wa LGBT wanakumabana  na ukatili na kubaguliwa kwa misingi ya kuwa walivyo, wanapoishi, na wanayempenda.”