Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zika sasa inatia wasiwasi zaidi kuliko wakati mwingine wowote: WHO

Zika sasa inatia wasiwasi zaidi kuliko wakati mwingine wowote: WHO

Zika inasalia kuwa hatari kubwa ya afya inayotia wasiwasi sana , ambayo inahitaji juhudi za kimataifa kusaidia wanawake kujilinda na maambukizi , amesema leo mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO.

Dr Margaret Chan, ameyasema hayo katika maandalizi ya kila mwaka ya baraza kuu la afya duniani litakaloanza wiki ijayo mjini Geneva. Amesema..

(SAUTI YA DR CHAN)

“Kadri tunavyofahamu zaidi kuhusu zika ndivyo tunavyozidi kupata hofu. Ni lazima niseme tena kwamba, hatari ya zika imekuwa ikibadilika. Miaka ya nyuma na bado inaendelea hadi leo, wengi walioambukizwa virusi vya zika wanapata maradhi madogo, wengine wanapata maradhi ya viungo Guillan Barré Syndrome,na muhimu zaidi ni wanawake wajawazito , hivyo tunapaswa kuelekeza msukumo wetu kwenye jinsi gani ya kutoa elimu muafaka, taarifa na huduma ili wanawake walindwe na mbu na wawe na fursa ya uzazi wa mpango wa kisasa endapo wataamua kuchelewa kupata ujauzito”.

Katika mkutano wa baraza kuu la afya ujao, nchi zote wanachama 194 zinatarajiwa kuamua endapo kuidhinisha wito wa Dr Chan wa dola milioni 160 wa ongezeko la ufadhili ili kutekeleza mikakati ya kuchukua hatua haraka kukabiliana na dharura za afya. Hadi sasa nchi 9 zimearifu kuathirika na viruzi vya zika kwa kina mama wajawazito na kujifungua watoto wenye vichwa vidogo.