Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dini na siasa watetea ukeketaji Guinea- Ripoti

Viongozi wa dini na siasa watetea ukeketaji Guinea- Ripoti

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imesema ukeketaji wanawake na watoto wa kike nchini Guinea unazidi kuongezeka licha ya kuharamishwa kupitia sheria za kitaifa na kimataifa.

Takwimu zinaonyesha asilimia 97 ya wanawake na wasichana huko Guinea wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamekeketwa na kitendo hicho hufanyika wakiwa na umri wa chini ya miaka 10.

Akizungumzia ripoti hiyo kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amesema cha kusikitisha sheria zipo lakini kutokana na hofu ya kutengwa na jamii au kutoolewa, wasichana na wanawake wanasaka kukeketwa.

Halikadhalika hakuna utashi wa kisiasa kusimamia sheria ambapo hata viongozi wa kisiasa na kidini wanaunga mkono mila hiyo potofu.Ripoti imetaka serikali kusimamia sheria kwani hakuna misingi yoyote ya kuhalalisha mila hiyo potofu.