Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo la kutokomeza Malaria linaweza kufanikiwa- WHO

Lengo la kutokomeza Malaria linaweza kufanikiwa- WHO

Mwaka mmoja tangu mkutano mkuu wa shirika la afya duniani, WHO kuazimia kutokomeza Malaria katika nchi 35 ifikapo mwaka 2030, hii leo shirika hilo limesema lengo hilo licha kuwa ni la juu bado linaweza kufanikiwa. Amina Hassan na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Amina)

Katika taarifa ya leo iliyotolewa sambamba na siku ya Malaria duniani, WHO imesema mwelekeo ni mzuri kwani mwaka 2015 nchi katika ukanda wa Ulaya hazikuwa na kisa hata kimoja cha Malaria tangu visa Elfu 90 mwaka 1995.

Hata hivyo changamoto imesalia barani Afrika ambako Dkt, Pedro Alonso, Mkurugenzi wa mpango wa Malaria WHO amesema kunahitaji uwekezaji mkubwa na wa dharura kutokomeza ugonjwa huo huku akipongeza nchi za Afrika zilizo kwenye mwelekeo sahihi.

(Sauti ya Pedro)

"Hatua imepigwa Afrika kwa umuhimu wa kipekee, na tunatarajia nchi kadhaa za Afrika kufanikiwa kutokomeza malaria kabisa, kwa kuondoa maambukizi katika miaka mitano ijayo. Nchi hizi ni pamoja na Algerian ambayo imekaribia, Botswana, Cape Verde, Comoro, Afrika Kusini na Swaziland.’’

WHO pia imetoa wito kwa utashi wa kisiasa katika uwekezaji wa mbinu za kukabili Malaria ikiwemo matumizi ya vyandarua vyenye dawa pamoja na majaribio zaidi ya chanjo dhidi ya Malaria hususan barani Afrika ili hatimaye ikifanikiwa iweze kusambazwa miaka ijayo.