Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aitaka Iran iache kuua wenye makosa ya dawa za kulevya

Zeid aitaka Iran iache kuua wenye makosa ya dawa za kulevya

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito kwa Iran ikomeshe mauaji ya watu wanaokabiliwa na makosa yanayohusu dawa za kulevya, hadi pale bunge la nchi hiyo litakapojadili mswada wa sheria mpya itakayoondoa moja kwa moja hukumu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya.

Wanaume watano waliuawa mwishoni mwa wiki iliyopita nchini Iran, watatu kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya, na wawili kwa makosa ya kuua.

Taarifa ya Kamishna Zeid imesema, katika kesi moja ya Rashid Kouhi, kulikuwa na hofu kuhusu jinsi mashtaka katika kesi hiyo yalivyoendeshwa, na masikitiko makubwa kuhusu alivyonyimwa haki yake ya kuomba rufaa.

Mwaka uliopita wa 2015, watu wapatao 966 waliuawa nchini Iran, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili. Wengi wa watu hao waliuawa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.